2016-07-12 14:00:00

Vatican inapania kufufua majadiliano na Chuo Kikuu cha Al Azhar


Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, tarehe 13 Julai 2016 ataondoka kuelekea Cairo, Misri, ili kutembelea Chuo Kikuu cha Al Azhar, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Professa Ahmad Al Tayyib, Imam mkuu wa Al- Azhar, hapo tarehe 23 Mei 2016.

Askofu Guixot ataambatana na Askofu mkuu Bruno MusarĂ², Balozi wa Vatican nchini Misri ili kuandaa mkutano pamoja na Dr. Mahmoud Hamad Zakzouk, Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni wakongwe kutoka Chuo Kikuu cha Al-Azhar na mkuu wa Chuo kikuu hicho! Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu Francisko analitaka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kuangalia mbinu mkakati zitakazotumika tena ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Baraza hili na Chuo kikuu cha Al- Azhar.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.