2016-07-12 07:08:00

Umuhimu na maana ya Altare!


Ibada ya Misa Takatifu ni kumbukumbu ya sadaka ambamo hudumishwa sadaka ya Msalaba, na karamu takatifu ya umoja katika Mwili na Damu ya Bwana. Lakini adhimisho la Sadaka ya Ekaristi Takatifu huelekezwa kwenye umoja wa ndani wa waamini na Kristo kwa njia ya komunyo. Kukomunika ni kumpokea Kristo mwenyewe aliyejitoa sadaka kwa ajili ya waja wake. Katekisimu ya Kanisa Kanisa Katoliki inafafanua kwamba, Altare, ambayo Kanisa lililounganika katika kusanyiko huizunguka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, yanaonesha mambo mawili ya fumbo moja.

Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara iliyotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kristo alijitoa kwa ajili ya ukombozi wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Altare ni sura ya mwili wa Kristo anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha umuhimu wa kuzunguka  Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa.

Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti amehudhuria katika mkutano uliofanyika Jijini London, Uingereza. Katika tafakari yake makini, alionesha na kukazia umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Baadhi ya maneno yake yalitafsiriwa vibaya na kuonekana kana kwamba, Kardinali Sarah anataka kuanzisha mageuzi mapya ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu, kwa kuangalia ukutani badala ya maadhimisho ya sasa ya kuwaangalia waamini kama ilivyozoeleka.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican, ameamua kufafanua kwa kina na mapana kuhusu mawazo ya Kardinali Sarah kwa kusema kwamba maelekezo yote ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yamebainishwa vyema kwenye Misale ya Waamini. Altare inapaswa kujengwa ikiwa imetenganishwa na ukuta, ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa kuweza kuizunguka. Altare ijengwe mahali ambapo panaonesha ukuu na umuhimu wa Altare katika Ibada. Mkazo unaotolewa kwa sasa anasema Padre Lombardi ni kufuata taratibu za kawaida zilizobainishwa.

Hakuna mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kuanzia kipindi cha Majilio kwa mwaka 2017 kama ambavyo baadhi ya watu walitaka kuwasaidikisha wengine kwa kutafsiri vibaya maneno ya Kardinali Robert Sarah. Hakuna mageuzi ndani ya mageuzi, maneno ambayo yalitumika wakati fulani na kuleta mpasuko katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.