2016-07-12 07:58:00

Kard. Monsengwo kumwakilisha Papa Francisko Kigali 9- 15 Sept. 2016


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawaalika waamini kulitafakari tena na tena fumbo la huruma ya Mungu lililofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani na kwamba, hili ni sharti la wokovu wa binadamu. Ni kwa njia ya huruma, Mwenyezi Mungu amewajia na kuwakomboa watu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba huruma ni daraja linalowaunganisha Mungu na binadamu na hivyo kuufungulia moyo mlango wa matamaini ya kupendwa daima na Mwenyezi Mungu, licha ya dhambi na ubaya wa moyo. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa kwa namna ya pekee, linahamasishwa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, badala ya kutumia ukali. Kanisa lioneshe kwamba ni mama mpendelevu, wenye uvumilivu na huruma kwa watoto wake. Mama Kanisa anapenda kuwasha moto wa upendo hata kwa watoto wake waliojitenga kwa sababu mbali mbali.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Mama Kanisa anapenda kutangaza na kushuhudia ujumbe wa kutia moyo; faraja, mapendo na matumaini. Kwa namna ya pekee, familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, ili kweli huruma na upendo wa Mungu uweze kuiambata familia ya Mungu Barani Afrika.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuthamini maadhimisho ya Kongamano la Huruma ya Mungu kwa Afrika na Madagascar, litakalotimua vumbi huko Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 9 - 15 Septemba 2016, amemteua Kardinali Laurent Pasinya Monsengwo kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya yatakayoratibiwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. SECAM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.