2016-07-11 07:50:00

Imani bila matendo hiyo ni butu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 10 Julai 2016 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao kwa njia ya matendo kwani imani bila matendo haifai kitu. Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati wa tafakari yake juu ya mfano wa Msamaria mwema aliyeonesha huruma kwa mtu aliyekuwa ameangukia mikononi mwa wanyang’anyi wakamtenda vibaya kiasi cha kumwacha akiwa taabani.

Hapa Baba Mtakatifu amewataka waamini kutowagawa watu kwa makundi ili kutambua jirani yao ni nani, bali jirani ni mtu yeyote anayehitaji msaada wao wa hali na mali. Mfano wa Msamaria mwema unaonesha mtindo wa maisha ambayo waamini wanapaswa kuufuta huku wakijitahidi kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya watu. Waamini waache kishawishi cha kuwagawa watu katika makundi, bali watu wengine katika shida na magumu yao waguswe na moyo wa ukarimu na upendo kutoka kwa waamini. Bila ya kuwa na mwelekeo kama huu, hapo mwamini atambue kwamba, kuna jambo ambalo si sawa katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Wasamaria ni watu ambao walidharauliwa sana na Wayahudi kutokana na ukweli kwamba wao hawakuwa ni wachamungu kadiri ya vigezo vya dini ya kweli. Lakini Msamaria ndiye aliyemwonea huruma Yule mtu aliyekuwa ameangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Mwalimu wa Sheria, Kuhani na Mlawi wakapita kando bila kuguswa na mahangaiko ya mtu Yule. Kutokana na mwelekeo huu, Yesu anaendelea kuwahamasisha wafuasi wake kutowagawa watu kwa makundi bali kuguswa na mahangaiko yao na kutenda kwa jicho na  moyo wa huruma kama alivyofanya Msamaria mwema. Hii ni changamoto kwa kila mwamini anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko kwani jirani ni mtu yoyote mwenye shida na magumu ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, imani inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma:kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji inayofumbata upendo wa kweli na furaha. Waamini wanapaswa kujiuliza ikiwa kama kweli imani yao inamwilishwa katika matendo au wamekuwa ni watu wa maneno matupu ambayo kamwe hayaachi kutika. Amewauliza ikiwa kama wanajisadaka na kujitosa kuwa majirani kwa watu wenye shida na mahangaiko: kiroho na kimwili au wamejiweka pembeni na hata wakati mwingine kuchagua ni nani jirani zao.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, wakati wa utimilifu wa nyakati, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ndicho kigezo msingi atakachotumia ili kutoa hukumu. Kumbe, huu ni wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha matendo ya huruma katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.