2016-07-11 07:58:00

Argentina inaadhimisha Jubilei ya miaka 200 ya Uhuru wake!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa, Jumapili tarehe 10 Julai 2016 ameadhimisha Siku ya Utume wa Bahari Duniani, kwa kuhimiza sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya mabaharia pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatia shime mabaharia pamoja na wavuvi wote wanaoendelea kujisadaka kila siku kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa, hata kama dhamana hii wanaitekeleza katika hali ngumu na mazingira hatarishi. Amemwomba Bikira Maria, Nyota ya Bahari awaangalie kwa jicho la tunza yake ya kimama Mabaharia pamoja na wavuvi wote duniani.

Baba Mtakatifu licha ya kutambua uwepo wa umati mkubwa wa mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia, alikumbuka kwa namna ya pekee umati mkubwa wa mahujaji wa familia ya Radio Maria kutoka Poland waliofanya hija ya mshikamano kutoka Jimbo kuu la Cravocia hadi Roma, hija ambayo kwa mwaka huu imeingia katika awamu ya ishirini na tano. Nchini Tanzania, Radio Maria, sauti ya Kikristo katika familia ya Mungu nchini Tanzania inajiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Radio Maria ilipoanzisha huduma ya Uinjilishaji kwa njia ya Radio nchini Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua pia uwepo wa watu wa familia ya Mungu kutoka Argentina ambao mwaka huu wanaadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu walipojipatia uhuru wao. Katika barua yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Argentina kusonga mbele kwa imani na matumaini; kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi unaofumbatwa katika unabii.

Baba Mtakatifu anawataka kuwa imara katika hija ya maadhimisho ya miaka mia mbili ya uhuru wao, huku akionesha uwepo wake wa karibu kwa wagonjwa, maskini, wafungwa na wale wanaojisikia pweke katika maisha yao, bila kuwasahau watu ambao hawana tena fursa za ajira. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; vijana wanaoathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Hawa wote ni watoto wa Argentina ambao wana makovu katika safari ya maisha yao, hivyo anawaalika kuwa na matumaini na kuendelea kutembea katika hija ya maisha yao, ili kufikia lengo kamili la maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.