2016-07-09 13:53:00

Askofu mkuu Michael Wallace Banach ateuliwa kuwa Balozi Cape Verde


Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu mkuu Michael Wallace Banach kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Cape Verde na ataendelea kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Senegel na mwakilishi wa kitume nchini Mauritania. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Banach alizaliwa kunako tarehe 19 Novemba 1962 huko Worcester, Masschussetts, Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 2 Julai 1988 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Kunako mwaka 1992 akaanza huduma za kidiplomasia mjini Vatican.

Tangu wakati huo, amekuwa ni mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Vienna. Tarehe 22 Februari 2013 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Papua New Guinea. Tarehe 27 Aprili 2013 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu. Amewahi pia kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Solomon.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.