2016-07-07 12:02:00

GdB House Tegeta: Ni kituo cha huduma na Uinjilishaji


Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu Kristo, Kanda ya Tanzania, C.PP.S kwa kusoma alama za nyakati na kutambua changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima wameamua kuwekeza katika mradi wa Jengo la biashara na huduma za kijamii, utakaoliwezesha Shirika kupata fedha ya kugharimia miradi mingine ya Uinjilishaji ndani na nje ya Tanzania.

Jengo hili maarufu kama “Gdb House” limejengwa katika eneo la Tegeta, Jijini Dar es Salaam na baada ya kubarikiwa na kufunguliwa rasmi, tarehe 6 Julai 2016 sasa limeanza kutoa huduma ya: Maduka na Ofisi; Fedha na Mikopo; Huduma za Kibenki ambazo zinatolewa na Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ajili ya kuwakomboa na kuwainua wanyonge. Hapa pia kunapatikana huduma za ushauri: kiroho na kimwili pamoja na huduma ya michezo kwa watoto wa eneo la Tegeta ambao kutokana na msongamano wa watu na makazi ya watu hawana tena mahali salama pa michezo!

Jengo hili limejengwa katika eneo la Kanisa la mwanzo ambalo baadaye liligeuzwa kuwa ni kituo cha vijana, kituo cha elimu na eneo la shimo la taka kutoka Tegeta sasa linatumika kama kituo cha biashara na maendeleo ya kijamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kushuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni eneo ambalo linapania kuwapatia watumiaji wake amani na utulivu wa ndani.

Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania amemshukuru Mungu pamoja na Wamissionari wote walioamua kujifunga mikanda kwa njia ya sala, sadaka na majitoleo yao, ndoto ya ujenzi na hatimaye kukamilika kwa jengo hili lililowekewa jiwe la msingi kunako tarehe 22 Aprili 2010 na Hayati Padre Joachim Ndelianarua, wakati huo akiwa ni Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.

Huu ni mradi ambao umekumbana na changamoto nyingi hata kiasi cha kuwakatisha Wamissionari wengi tamaa, lakini “Kamanda” Padre Thomas Wambura akasimama kidete usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, mradi huu unakamilika kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Nia njema ya Wamissionari kwa njia ya ushirikiano na viongozi mbali mbali wa Shirika, wafadhili pamoja na waamini walei walioshirikisha: akili, taaluma, weledi, ujuzi na nguvu zao, “Jengo la GdB” limefunguliwa na sasa linacharuka kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Jijini Dar es Salaam katika ujumla wake.

Padre Chesco Msaga anawapongeza na kuwashukuru waamini walei nchini Tanzania wanaoendelea kulisaidia Kanisa na Shirika kwa namna ya pekee ili kuweza kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Padre Msaga anasema, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Mkombozi anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kutumia huduma za Benki ya Mkombozi ambazo zimeboreshwa na kusogezwa karibu zaidi na wananchi wa eneo la Tegeta, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania wengi.

Kwa upande wake “Kamanda” Thomas Wambura amesema ujenzi wa kituo hiki unakwenda sanjari na sera na mikakati ya Kanisa katika kujitegemea na hatimaye, kuchangia maboresho ya huduma zinazotolewa na Kanisa: kiroho na kimwili katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Kituo kitaendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaojikita katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai, Huruma ya Mungu pamoja na familia. Faida itakayopatikana kutokana na mradi huu itatumika katika kugharimia huduma za kiroho na kijamii zinazotolewa na Wamissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania.

Padre Chesco Peter Msaga kabla ya kubariki na hatimaye kuzindua Jengo hili aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu na Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ambalo baada ya kuadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1815 – 2015, sasa Wamissionari hawa kwa mwaka 2016 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Uwepo wa Shirika hili nchini Tanzania na Miaka 25 tangu Mapadre wa kwanza wazalendo walipopewa Daraja Takatifu la Upadre, kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 18 Agosti 2016 huko Manyoni, Jimboni Singida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.