2016-07-06 09:02:00

Utume wa sala kwa njia ya video wapata mafanikio makubwa!


Padre Frèdèric Fornos, Mkurugenzi wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, tangu mwezi Januari 2016 nia za Baba Mtakatifu Francisko zimekuwa zikiandamana na ujumbe kwa njia ya video, hali ambayo hadi sasa imepata mafanikio makubwa. Ujumbe huu umeweza kuwafikia Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema pasi na ubaguzi. Kwa njia ya ujumbe kwa video watu wengi wanajisikia kwamba, baba Mtakatifu Francisko yuko karibu katika maisha na utume wake.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miezi sita, zaidi ya watu millioni kumi wanaotumia mitandao ya kijamii wameweza kusikiliza na kuona ujumbe wa nia za Baba Mtakatifu Franciko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ujumbe huu ambao ni mfupi lakini unagusa mawazo msingi, unawasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuendelea kuwa karibu zaidi na Kanisa kwa njia ya sala.

Padre Fornos anaendelea kufafanua kwamba, utume wa sala kwa njia ya mitandao ya kijamii unaendelea kupata mafanikio makubwa hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Hadi sasa kuna kikundi cha “Vijana wa Ekaristi Takatifu” kwa njia ya mitandao ya kijamii kinachoundwa na vijana zaidi ya millioni moja. Kwa vijana ujumbe kwa njia ya video imekuwa ni nafasi kwa vijana wengi kukaa karibu na Baba Mtakatifu, ili kumsaidia na kumsindikiza kwa njia ya sala na sadaka yao. Imekuwa ni nafasi ya kufahamu mahangaiko ya Kanisa kwa watu mbali mbali na kwa njia hii, vijana wengi wamejikuta wakipyaisha maisha yao ya kiroho!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unawapatia waamini nafasi ya kusikiliza, kuona na kusoma nia zake, tayari kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anazungumza na kuwashirikisha watu kile kinachofumbatwa katika undani wa moyo wake kwa ajili ya maskini na watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Kwa njia ya maneno na jicho la Baba Mtakatifu, watu wengi wanaweza kujionea majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika maisha yake ya kila siku. Hawa wengi wamesaidiwa kuona na kuguswa na mahanagiko ya jirani zao, kielelezo makini cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya watu: kiroho na kimwili.

Utume wa Sala unapenda kuwasaidia waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya sala kwa njia ya matumizi ya mitandao ya kijamii, inayoweza kuwafikia watu wengi mahali walipo. Mwezi Julai, utume wa Sala unazindua matumizi “Click to Pray”, huduma itakayowasaidia waamini kusali kwa njia ya mitandao yao ya kijamii, huku wakiungana na Baba Mtakatifu. Itakumbukwa kwamba, ni ana ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa umesambaa kwenye mitandao yote ya kijami. Kwa sasa lugha zinazotumika ni: Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiitalia kinaingizwa mwezi Julai. Ujumbe huu unatumia dakika 4:50. Hii inaonesha kwamba, watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwa kusali na kutafakari, ili kuzama zaidi kwenye nia za Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.