2016-07-06 08:35:00

Papa- nguvu za kijeshi haziwezi kuleta amani Syria isipokuwa mazungumzano


Baba Mtakatifu Francisko,  kwa njia ya video alitoa ujumbe wenye kuunga mkono kampeni iliyozinduliwa na Shirika la Misaada Katoliki la Kimataifa ( Caritas Internationalis),  inayohimiza kurejesha amani nchini Syria. Katika ujumbe wake, Papa Francisko ametaja wazi kwamba, inawezekana kuwa na amani Syria ,si kwa  kutumia njia za kijeshi bali kwa njia ya mazungmzano ya kisiasa,  yanayopaswa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na kutembea pamoja katika ujenzi wa serikali ya muungano na umoja wa kitaifa kwa taifa la Syria.

Papa alieleza na kuonyesha jinsi matatizo ya vita vya Syria ambavyo kwa sasa viko mwaka wa tano huutia simanzi moyo wake.. hasa kutokana na ukweli kwamba ni  hali ya mateso isiyo na kifani kwamba,  watu wengi wa  Syria wamekuwa wahanga wa mateso, wakilazimishwa kuishi chini ya mitutu ya bunduki na mabomu, vinginevyo ni lazima kuikimbia nchi yao wakiwa watupu, kukimbilia nchi nyingine au katika maeneo mengine wanakoona wanaweza salimisha maisha yao. Kwa mtazamo huo Papa huwafikiria wakristo wa eneo hilo, na hivyo huungana na wote wenye mapenzi mema, kutoa msaada wote unaowezekana kwa Wahanga hao , ili waweze kukabiliana na dhuluma na kubaguliwa.

Katika Ujumbe huu  Papa amewaomba  waamini wote na wale wanaohusika na utoaji wa misaada Katoliki (Caritas) wote wapanie kujega jamii ya haki. Ameonyesha kujali kwamba, wakati watu wanateseka kikweli , kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kununua silaha na kuzisambaza kwa wapiganaji.  Na  baadhi ya nchi zinazosambaza silaha hizo pia ni miongoni mwa wale wanaoshiriki katika majadiliano ya amani. Papa kwa masikitiko amehoji kwa vipi unaweza mwamini mtu anayekubebeleza kwa mkono wa kulia na wakati huohuo kukuchapa kofi kwa mkono wa  kushoto?

Papa ametoa wito kwa watu wote, watu wazima na vijana,kuuishi mwaka huu Mtakatifu wa Huruma na shauku kubwa ya kutaka kuzishihnda tofauti na kutangaza kwa nguvu kwamba amani nchini Syria inawezekana! Amani  Syria inawezekana!

Kwa ajili hii, Papa amesema, binadamu wote tunatakiwa kukumbatia Neno la Mungu linalotuambia” Mimi ninaijua mipango niliyokuandalieni ninyi” “Ni mipango ya amani na si uharifu ni mipango ya siku za baadaye iliyojazwa  matumaini”(Yeremia, 29.11)

Huu ni mwaliko unaotutaka kusali kwa ajili  ya amani nchini Syria na kwa ajili ya watu wake ,  ni sala ya mkesha na ni wakati wa kuwa na utambuzi wa kuanzisha juhudi mpya katika vikundi , parokiani na katika jumuiya kwa ajili ya kueneza ujumbe wa amani, ujumbe wa umoja na matumaini. Papa alisisitiza kwamba, kazi za amani hufuatiwa na sala. Na hivyo anawaalika wale wote ambao hushiriki katika mazungumzo ya amani kuchukua makubaliano hayo kwa makini na kufanya kila jitihada ili kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

Na amemtaka kila mmoja kutambua kwamba , hakuna jawabu la kijeshi linalo weza rejesha amani  Syria, isipokuwa  ufumbuzi wa kisiasa. Kwa hiyo ni lazima jumuiya ya kimataifa isaidie kufanikisha mazungumzo ya amani kuelekea kwenye ujenzi wa serikali ya umoja wa kitaifa. Papa ameeleza katika ujumbe wake na kuwaomba wote kuunganisha nguvu  katika ngazi zote , kwa ajili ya kuhakikisha amani inapatikana kwa taifa pendwa la Syria. Na kwamba kufanikisha hili, itakuwa ni mfano mkubwa wa huruma na upendo wa jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya mazuri ya wote.  Papa ameiweka kampeni hii chini ya ulinzi wa Mama Maria Mtakatifu sana. 








All the contents on this site are copyrighted ©.