2016-07-05 09:27:00

Miaka 30 Makomandoo wa Israeli walipovamia Uwanja wa Entebe!


Uganda inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 30 tangu Makomandoo wa Israeli walipovamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebe ili kuokoa mateka 100 kutoka Israeli. Katika tukio hili lililowaacha watu wengi wakiwa wameshika tama, mateka 100 waliweza kuokolewa, lakini wanajeshi 20 wa Uganda waliuwawa pamoja na wateka nyara saba. Yonatan Netanyahu kutoka Israeli ndiye pekee aliyeuwawa katika operesheni hii.

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa Israeli, Siku ya Jumatatu, tarehe 4 Julai 2016 ameanza ziara ya kiserikali kwa ajili ya kumbu kumbu hii huko Uganda na anatembelea pia Kenya, Ethiopia na Rwanda kwa lengo la kutaka kuimarisha uhusiano kati ya Israeli na Bara la Afrika. Waziri Mkuu Netanyahu anakuwa ni kiongozi wa ngazi za juu kutoka Israeli anayetembelea Bara la Afrika takribani baada ya miaka 30.

Itakumbukwa kwamba, uhusiano kati ya Israeli na Bara la Afrika katika miaka 1960 wakati nyingi nchi zikijipatia uhuru wake ulikuwa mzuri sana. Israeli ilikuwa ni mdau mkubwa wa mchakato wa maendeleo hususan katika ujenzi wa miundo mbinu, ulinzi na usalama. Kwenye miaka ya 1970 mahusiano haya yakaanza kulega lega sana kutokana na mashinikizo ya Jumuiya ya Kimataifa. Israeli inataka kuimarisha uhusiano wake na Bara la Afrika.

Israeli inataka kuwekeza kiasi cha dolla za kimarekani millioni 13 katika mchakato wa maendeleo endelevu hususan katika sekta ya: kilimo, afya, ulinzi na usalama ili kuweza kukabiliana na vikundi cha kigaidi kama vile Boko Haram na Al Shabab ambavyo vinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Nigeria, Kenya, Ethiopia, Uganda na Cameroon zinatarajia kupata msaada huu kutoka Israeli ili kupambana na vitendo vya kigaidi. Lakini Israeli pia inashutumiwa na Jumuiya ya Kitaifa kwa kutokuwa na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ndani ya mipaka yake na wala hawana ruhusa ya kupata fursa za ajira nchini humo.

Wachunguzi wa mambo ya kimataifa wanasema, pengine Uganda na Rwanda zinaweza kuwa ni nchi mbili za Kiafrika zitakazotoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika wanaoishi kwas asa nchini Israeli, ili hatimaye kupata msaada wa kijeshi kutoka Israeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.