2016-07-04 11:16:00

WCC 2018 kufanya mkutano wake mkuu Arusha, Tanzania


Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuanzia tarehe 8 - 13 Machi 2018 litafanya mkutano wake wa kimataifa mjini Arusha, Tanzania utakaoongozwa na kauli mbiu “Kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu: Wito wa mageuzi ya ufuasi”. Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 700 kutoka kwenye Makanisa mbali mbali duniani na Kanisa la Kiluteri la Kiinjili Tanzania ndilo litakalokuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa mara ya mwisho lilifanya mkutano wake Barani Afrika kunako mwaka 1958 huko Ghana. Wazo la Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuadhimisha mkutano wake mkuu nchini Tanzania liliwasilishwa hivi karibuni na Askofu Geevarghese Mor Coorilos, Mratibu wa Tume ya Utume na Uinjilishaji Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake uliokuwa unafanyika hivi karibuni huko Trondheim, Norway.

Wajumbe wa mkutano huu wamekubaliana kimsingi kwamba, Bara la Afrika ni kati ya Mabara ambayo kwa sasa yanaonesha ari na moyo mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji na kwamba, umefika wakati kwa Makanisa ulimwenguni kushuhudia imani inavyoendelea kukuzwa na kudumishwa Barani Afrika. Kutokana na changamoto hii, wawezeshaji wakuu wakati wa mkutano huu watapaswa kutoka Barani Afrika ili kushirikisha tunu msingi za maisha na utume wa Makanisa Barani Afrika. Hii itakuwa ni nafasi ya kupembua kwa kina na mapana mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Tangu kunako mwaka 1910 Baraza la Makanisa Ulimwenguni lilipoanzishwa, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa sasa kipaumbele si kuwaongoa watu, bali ni huduma ya upendo na mshikamano wa dhati kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, njaa, magonjwa na mipasuko ya kijamii. Huu umekuwa ni wakati wa kujikita zaidi katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu dhidi ya utamaduni wa kifo, kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.

Hapa kinachotakiwa kwa sasa ni Uekumene wa huduma unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa. Makanisa yanapaswa kutoka kimasomaso ili kulinda  na kutunza mazingira nyumba ya wote kwani waathirika wa mabadiliko ya tabianchi ni wengi sana duniani na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: haki msingi za binadamu utu na heshima ya binadamu kwa kujikita katika Injili ya uhai na utawala bora.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, leo hii watu wanaishi katika ulimwengu ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu, kumbe, mkutano huu utakuwa ni fursa ya kupembua maana ya utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kama mitume na wafuasi wa Kristo wanapaswa kuendelea kumuiga Kristo Yesu kwa kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wafuasi wa Kristo wanapaswa kubadilika, wanapaswa kuongoka na kuwa watu wapya daima kwa kujifunza kutoka kwa watu wanaowahudumia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, mkutano huu utawashirikisha wajumbe wa Baraza hili pamoja na wawakilishi kutoka katikaMakanisa ya Kipentekosti na Kanisa Katoliki ambayo si mwanachama  wa Mabaraza ya Makanisa Ulimwenguni. Lengo ni kushirikiana kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka kutoka katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kushuhudia imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.