2016-07-04 09:54:00

Umoja unawezekana!


Kongamano la nne la Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya “Together 4 Europe” limehitimishwa huko Baria, Munich nchini Ujerumani, hapo tarehe 2 Julai 2016. Viongozi mbali mbali wa Makanisa wametoa ujumbe kuonesha kwamba, kwa njia ya umoja na mshikamano, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza katika mahusiano na mafungamano ya kijamii, Umoja  wa Ulaya ni jambo linalowezekana.

Huu ndio wakati uliokubalika wa kushikamana ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazolikabili Bara la Ulaya ili kushuhudia jamii inayojikita katika ukarimu na mshikamano na maskini; kwa kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana; kwa kuvuka kuta za utengano wa wazi na ule wa mawazo pamoja na kushirikishana karama na mapaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ni changamoto pevu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa kongamano hili.

Wajumbe katika tamko lao baada ya maadhimisho haya wanakaza kusema, miaka 500 ya utengano kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri inatosha sasa Wakristo wote kwa pamoja  wanataka kuona umoja wa Kanisa. Akizugusia kuhusu umoja wa Kanisa, Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha Kitume cha Wafokolari, amesisitiza kwamba, mchakato wa umoja wa Wakristo ni amri kutoka kwa Kristo mwenyewe aliyewaombea mitume wake ili wawe wamoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Wote wanakumbushwa kwamba, ni watoto wa Mwenyezi Mungu wanaounda familia moja ya binadamu, kumbe umoja ni jambo ambalo linawezekana kabisa na wala si kitu cha kufikirika. Hili ndilo linapaswa kuwa ni lengo la Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema. Kila mwamini anapaswa kujitosa kimasomaso ili kuwa kweli ni shahidi na chombo cha umoja na mshikamano, ili kupata mwelekeo mpya wa Bara la Ulaya linaloshikamana zaidi. Waamini wakifanikisha azma hii, hata mchakato wa umoja wa Kanisa utaongeza kasi zaidi kwa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Kwa upande wake Gerhard Pross amekazia umuhimu wa kujenga umoja katika tofauti ambazo zimepatanishwa. Andrea Riccard, muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anasema, wakati wa ujenzi wa kuta za utengano umekwisha, sasa watu wapanie kujenga madaraja yanayowaunganisha watu kwa maneno na matendo. Viongozi wengi wa Makanisa wamekazia kwa namna ya pekee, majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika ushuhuda wa huduma ya upendo; na Uekumene wa damu, unaoshuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, kifungo cha umoja na mshikamano kati ya Wakristo wote.

Kardinali  Reinhard Marx anasema, mwono wa pamoja wa Bara la Ulaya lililoungana ni mkubwa zaidi ikilinganishwa n ana woga na wasi wasi wa kuishi pamoja kama Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, changamaoto ni kuendelea sasa kujikita katika mchakato wa upatanisho ili kuishi katika umoja unaotambua na kuthamini utofauti ambao kimsingi ni utajiri wa familia ya Mungu hapa duniani. Kwa kuheshimiana na kuthaminiana, waamini wawe na ujasiri wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene katika ukweli na uwazi, daima wakitafuta mafao ya wengi, haki, amani na mshikamano wa dhati kabisa kati ya watu. Upatanisho ni neno msingi kwa wakati huu Barani Ulaya ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoibuka usiku na mchana.

Katika kongamano hili la siku mbili, wajumbe wamepata pia fursa ya kujadili kwa kina na mapana masuala ya: majadiliano ya kidini na kiekumene; ushirikishwaji na mshikamano; ndoa na familia; uchumi na mafao ya wengi. Kardinali Walter Kasper amekaza kusema upatanisho wa kweli ni changamoto kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo. Hapa kunahitajika msamaha, ili kusonga mbele katika hija ya pamoja kuelekea umoja wa Kanisa.

Lakini ikummbuke kwamba, majadiliano ya kidini na kiekumene yanapaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku na wale si kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majadiliano ya ngazi ya juu, ambayo mara nyingi yanaishia kuwekwa kama kumbu kumbu kwenye Makabati ya Makanisa. Majadiliano ya kweli yanafumbata maisha ya watu wa kawaida kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wakati wa raha na shida. Bado kuna haja ya kuendeleza majadiliano kati ya sayansi na dini pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Bara la Ulaya bado lina nafasi ya kuchangia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa umoja katika tofauti, hali ambayo inaweza kushuhudiwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.