2016-07-04 07:21:00

Kanisa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Gazeti La Nacion linalochapishwa nchini Argentina anampongeza na kumshukuru Papa mstaafu Benedikto XVI kwa ujasiri wa maamuzi magumu yaliyoleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ameonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa Kanisa na kwamba, uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani hauna uhusiano wowote na masuala binafsi. Ameonesha upendo kwa Kanisa na kwamba, afya yake ni nzuri, ingawa umri unaendelea kusonga mbele kiasi cha kumsababishia pia kutembea kwa shida! Lakini, bado ana kumbu kumbu makini sana.

Baba Mtakatifu anasema hana shida yoyote na Rais Mauricio Macri wa Argentina na kwamba, yeye si mtu anayependa kinzani na mipasuko katika maisha ya watu. Rais Macri ni kiongozi anayetoka katika familia nzuri. Anakumbuka kwamba, walau wakati mmoja waliwahi kusigana na Rais Macri alipokuwa Gavana wa Mji wa Buenos Aires kwa muda wa miaka sita. Lakini lilikuwa ni jambo la kawaida na kwamba, matatizo na changamoto nyingine zilizojitokeza zilijadiliwa katika faragha na kuheshimiwa na kwamba, hana sababu ya msingi ya kumshutumu Rais Mauricio Macri wa Argentina.

Kuhusu mazungumzo yake na Mama Hebe de Bonafini, kiongozi wa wanawake wa “Plaza de Mayo” ambaye mwanzoni alikuwa ni mpinzani mkubwa wa Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa nchini Argentina kwa kumshutumu kwamba, alikuwa anashirikiana na Serikali kuwanyanyasa wananchi wa Argentina, mwishoni amekiri kwamba shutuma hizi hazikuwa na ukweli wowote na kwamba, alikosea kumshutumu Baba Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, mazungumzo yake na Mama Hebe de Bonafini, kilikuwa ni kitendo cha kuomba msamaha ambao Baba Mtakatifu anasema, alimpatia kwani hii ni haki ya kila mtu.

Baba Mtakatifu anasema, huyu ni mwanamke ambaye watoto wake wawili waliuwawa kikatili kumbe, uchungu wa mwana aujuaye ni mama! Baba Mtakatifu anakaza kusema, mbele ya mateso na mahangaiko ya watu, anapiga magoti kwa heshima kuu na kwamba, hajali kile ambacho huyu mama alisema juu yake wakati ule, sasa ni wakati kufungua ukurasa mpya na kusonga mbele kwa matumaini zaidi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Vatican ina msemaji mkuu mmoja tu na wala hakuna msemaji mwingine mbadala wa Vatican nchini Argentina au kwingine kokote duniani. Msemaji mkuu wa Vatican ndiye sauti pekee ya Papa na kwa sasa ni Padre Federico Lombardi. Kuhusu Mfuko wa Kipapa wa Scholas Occurrentes ulioanzishwa na Papa Francisko takribani miaka kumi na mitano iliyopita anasema kuanzia sasa Mfuko wa Schola Occurrentes hautapokea fedha kutoka serikalini, ili kuweza kuwa makini katika kuratibu na kusimamia rasilimali fedha ya mfuko huu. Fedha ya Serikali itumike kwa ajili ya kuwasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa Argentina. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anatamani kuona Kanisa ambalo liko wazi, linaloeleweka na kusindikiza familia ambazo zinaogelea katika dimbwi la shida na magumu ya maisha, ili hatimaye, ziweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.