2016-07-03 11:15:00

Rais wa Ghana ashambuliwa kwa mawe!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana limesikitishwa sana na vitendo vya kihuni walivyofanya baadhi ya wananchi katika mkoa wa Ashanti, Kusini mwa Ghana wakulitupia mawe gari la Rais John Dramani Mahama, hivi karibuni wakati alipokuwa anatembelea mkoani humo. Taarifa za Polisi zinaonesha kwamba, watu wengi walijeruhiswa kutokana na shambulizi hili na kwamba, baadhi ya watu wanashikiliwa na Polisi kutokana na shutuma hizi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linasema, vitendo hivi vinasikitisha sana na Kanisa linavilaani kwa nguvu zote na kuwataka wale walioshiriki katika mashambulizi haya kujionea aibu ya mwaka na wanatakiwa kuomba msamaha. Hii inatokana na ukweli kwamba, vitendo hivi amefanyiwa Rais ambaye tangu aingie madarakani ameonesha kuwa ni mtu wa amani anayejikita zaidi katika upatanisho na umoja wa kitaifa. Lakini mbaya zaidi, mashambulizi haya yameelekezwa kwa mkuu wa nchi, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utovu wa nidhamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana katika tamko lililotiwa mkwaju na Askofu Joseph Osei- Bonsu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linakaza kusema, watu wote waliohusika katika tukio hili wachukuliwe hatua za kinidhamu ili liwe ni fundisho kwa watu wasiopenda amani na utulivu. Wachunguzi wa mambo wanasema,  pengine hasira za wananchi zinatokana na ukweli kwamba, hivi karibuni Rais John Dramani Mahama wa Ghana amepokea zawadi ya gari lenye thamani ya dolla za kimarekani 25,000 kama takrima kutoka kwa kampuni moja, ili Serikali iweze kutoa tenda ya kutengeneza barabara na ujenzi wa uzio wa eneo la Ubalozi wa Ghana nchini Burkina Faso. Msemaji wa Serikali amekanusha shutuma hizi na kusema kwamba, zawadi ya gari aliyopewa Rais Mahama ni kwa ajili ya matumizi ya Serikali kwa wale watakaokuwa kwenye msafara wa Rais na wala si kwa ajili ya matumizi binafasi kama inavyodaiwa. Rais naye kwa upande wake anaendesha kampeni dhidi ya rushwa naufisadi nchini Ghana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.