2016-07-02 07:52:00

WCC: Shikamaneni kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo


Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni huko Trondheim, Norway, inasema, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayaalika Makanisa wanachama 350 kuhakikisha kwamba, yanajifunga kibwebwe ili kupambana na hatimaye, kutokomeza biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Injili ya Kristo iwe ni mfano na changamoto ya kuwahamasisha waamini  kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kupambana na uhalifu huu dhidi ya ubinadamu katika maeneo yao. Ikumbukwe kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni changamoto ya kimataifa inayonyanyasa utu na heshima ya binadamu, kwa kuwanyima watu uhuru na kuendelea kuwadhalilisha kwa kuwafanyisha kazi za suluba; kwa kuwatumbukiza katika biashara na utalii wa ngono bila kusahau biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Viongozi wa Makanisa pamoja na waamini katika ujumla wao wawe mstari wa mbele kushirikiana na vyombo vya sheria ili kupambana na biashara hii haramu, inayosababishwa na umaskini mkubwa watu, uchu wa mali na utajiri wa haraka. Wajumbe wa Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni inawataka Wakristo wote kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima, haki na amani kwa kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinazonesha kwamba kuna zaidi ya watu millioni 2. 5, kati ya wao asilimia 75 ikiwa ni wanawake na wasichana wenye umri chini ya miaka 18 ambao wametumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Changamoto hii ni kubwa huko Amerika ya Kusini na kwa sasa hali inaendelea kuwa mbaya hata kutoka Barani Afrika. Ili kukomesha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kuna haja ya kushikamana kupambana na changamoto hizi, huku wakiwa wanaongozwa na Injili ya Kristo, ili kusaidia mchakato wa kuragibisha mapambano haya pamoja na kushirikiana na taasisi pamoja na vyombo vya sheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.