2016-07-02 07:14:00

Jiji la Roma linapaswa kuwa ni mfano bora wa maadili na tunu za kiroho


Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza amekutana na kuzungumza na Meya mpya wa Jiji la Roma Dr. Virginia Raggi, Ijumaa tarehe 1 Julai 2016. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Dr. Raggi amekiri kwamba, hii ni mara yake ya kwanza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko aliyeonesha utu na ubinadamu unaofumbatwa katika maisha na utume wake; mambo ambayo yamemgusa kwa namna ya pekee kabisa.

Dr. Raggi anakaza kusema, Jiji la Roma linapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kimaadili na katika maisha ya kiroho, lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio ambayo yanaashiria kumong’onyoka kwa kanuni maadili, uaminifu, ukweli na uwazi katika kulinda na kudumisha mafao ya wengi. Hii inatokana na ubinafsi uliooneshwa na baadhi ya viongozi waliopewa madaraka na umma. Umefika wakati kwa viongozi wa Jiji la Roma kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho zinapewa kipaumbele cha pekee katika huduma kwa familia ya Mungu.

Dr. Raggi anatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Kanisa katika huduma kwa familia ya Mungu Jijini Roma: kiroho na kimwili, mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na ujenzi wa jamii inayojikita katika mshikamano, umoja na udugu. Utawala wa sheria unapaswa kupewa umuhimu wa kwanza katika masuala ya uongozi.

Dr. Raggi anaendelea kufafanua kwamba, Jiji la Roma linapaswa kuonesha upendo, mshikamano na ukarimu kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao. Lakini kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya viongozi wanaotumia fursa ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kujitajirisha wenyewe badala ya kuwahudumia walengwa. Fedha inapaswa kuhudumia watu na wala si kinyume chake. Katika mchakato wa kubana matumizi, kuna haja ya kuboresha huduma hasa kwa watoto wadogo na familia; kwa walemavu na maskini, ili wote waweze kufaidika na huduma ya uongozi bora sanjari na maboresho ya usafiri. Kimsingi, wananchi wote wanawajibika katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya Jiji la Roma, jambo ambalo halina budi kwenda sanjari na utawala bora unaozingatia mahitaji ya wananchi wake, ili haki iweze kutendeka na watu kuishi katika hali ya amani na utulivu.

Kuhusu maandalizi ya mashindano ya Michezo ya Olympic kwa mwaka 2024, Dr. Virginia Raggi, Meya wa Jiji la Roma anasema, hiki si kipaumbele cha wananchi wa Roma kwa wakati huu. Hakuna sababu ya msingi ya kuweza kuwatishwa gharama wananchi wa Roma kwa ajili tu ya kutaka kuwa wenyeji wa mashindano ya michezo ya Olympic kwa mwaka 2024. Jiji la Roma kwa sasa lina deni kiasi cha Euro billioni 13 kutokana na matumizi ya dharura, kumbe si haki wana suala la kimaadili kuendelea kuwatisha wananchi wa Roma mzigo wa madeni utakaolipwa kwa miak 20, 30, 40 na kuendelea. Hapa kanuni maadili na haki vinazingatiwa na kupewa kipaumbele cha kwanza anasema Dr. Virginia Raggi katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.