2016-06-30 14:44:00

Wanasiasa lindeni na kudumisha tunu msingi za ndoa na familia!


Kardinali  Juan Luis Ciprian, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, nchini Perù anawataka viongozi wa serikali pamoja na vyama vya kisiasa wanaowania madaraka nchini humo katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Wabunge uliofanyika mwezi Aprili, 2016 kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kujenga na kudumisha haki msingi za maisha ya kifamilia; kwa kutoa fursa kwa wazazi kutoa elimu na malezi bora kwa watoto wao kadiri ya imani na utashi wao na kamwe wasiwavuruge kwa sera na mikakati inayopania kukumbatia utamaduni wa kifo.

Waamini na watu wenye mapenzi mema, wawe makini kuwachagua viongozi wenye mielekeo sahihi ya maisha, maadili na utu wema; watu wanaoweza kusimamia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; utu, heshima na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Ikumbukwe kwamba, familia ni taasisi ya kwanza kabisa inayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na baadaye masuala ya kisiasa. Serikali na sera za uchumi zisizotoa msukumo wa pekee katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ni hatari kwa taifa hilo.

Kardinali Juan Luis Ciprian anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Perù kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika huruma na upendo wa Mungu; haki, furaha, ukarimu na msamaha wa dhati. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kukaza uso wake kama gumegume ili kusimamia tunu msingi za Injili ya familia, hata pake ambapo itabidi kuteseka, litateseka, lakini lazima litangaze na kushuhudia ukweli, uzuri na utakatifu wa ndoa na familia.

Kardinali Ciprian anasikitika kusema kwamba, kwa sasa kuna watu wanaoendelea kutangaza na kushabikia masuala ya usawa wa kijinsia na kusahau kwamba, mwanaume na mwanamke wameumbwa ili kukamilishana na kusaidiana katika hija ya maisha yao. Kutotambua na kuthamini tofauti za kijinsia ni hatari kubwa kwa ustawi na maendeleo ya binadamu. Mtoto ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi ambao wanapaswa kutekeleza dhamana hii kwa unyofu na uchaji, wakiwa tayari kuwahudumia na kuwalea watoto wao, ili waweze kuwa raia wema na watakatifu kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kuna sera na mikakati ya makusudi kabisa inayotaka kubomoa msingi wa ndoa na familia, kwa kuwaaminisha watu juu ya uhuru usiokuwa na mipaka; uhuru usiokuwa na tija wala mashiko; uhuru unaokumbatia utamaduni wa kifo, tayari kumwangamiza binadamu. Kanisa halina budi kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya familia kwa kupambana na ubinafsi, uchoyo pamoja na tabia ya watu kukengeuka na kutopea katika dhambi kwa kisingizio cha uhuru binafsi! Hakuna uhuru wa kweli usiokuwa na mipaka, nidhamu, utu na maadili mema.

Kutokana na mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa zinajikuta ziko njia panda. Watu wengi wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa shughuli za kiuchumi; kwa kutafuta fedha na mali, kiasi hata cha kusahau dhamana na majukumu ya kifamilia.

Ni watu wanaondoka asubuhi na mapema ili kutafuta riziki ya kila siku, wanarejea nyumbani kumekuchwa, huku wakiwa hoi bin taaban! Hapa familia inakosa nafasi ya kukutana na kuendelezana katika huruma, mapendo, umoja na mshikamano wa dhati. Familia zisaidiwe kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.