2016-06-30 15:32:00

Mnatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema!


Utume wa Kanisa unafupishwa kwa maneno ya Kristo katika Injili ya Marko anaposema “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa” (Mk 16:15 – 16). Utume huu si jambo jingine bali ni uendelezaji wa habari njema ya wokovu ambayo Bwana wetu Yesu Kristo kwa hiyo aliutwaa ubinadamu wetu na kukaa katikati yetu. Habari hiyo ni “kuwahubiria maskini habari njema ... kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa (Lk 4:18 – 19). Hii inamaanisha kwamba utume wa Kanisa unapaswa kujikita katika kumwangalia mwanadamu aliyejeruhiwa, kumganga na kumfanya apate nafuu na kuiona tena huruma ya Mungu. Wajibu huu kama tunavyosisitiziwa sana katika mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu huonekana vizuri zaidi kwa kuwaangalia wale waliosukumiziwa pembezoni na ambao sauti zao haziwezi kusikika. Mfano wa hawa ni yatima, wajane na wanyonge wengi katika jamii ya mwanadamu.

Somo la Injili la Dominika hii lina tuwekea tukio hilo la kutumwa. Yesu anawatuma watu sabini mbili wamtangulie kule ambapo anakusudia kwenda. Hii ni ishara nzuri ya utume wa Kanisa kwamba unaanzia kwa Mungu mwenyewe na lengo lake ni kwenda kumfanyia makao huko anapotuma. “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake”. Huu ndiyo wito kwa Kanisa katika kuwaunda watenda kazi ambao watatumwa kuvuna shambani mwa Bwana. Jamii ya mwanadamu inayo mahitaji mengi ambayo bado yanahitaji kuipokea habari njema, kufunguliwa na kupewa mwanga na zaidi wanahitaji kuuona uso wa Mungu wenye huruma. Jukumu linalotolewa kwa Kanisa ni kuutangaza Ufalme wa Mungu hapa duniani, ufalme ambao ni wa amani, ufalme wenye nguvu, ufalme wa haki na wa milele (Rej Is 9:6 – 7). Kanisa linatumwa kufanya utume wa kuukarabati ubinadamu uliochakaa.

Somo la Injili linaendelea kuonesha mazingira halisi ya utume huo. “Enendeni, angalieni, nawatuma kama Kondoo kati ya mbwa-mwitu”. Muktadha huu unatudai sisi kama Kanisa kuwa na ujasiri na uangalifu. Ni mazingira kinzani ambapo tunaelekezwa kuutekeleza huu utume wetu. Adui shetani hana raha tena kwa sababu ya Ufalme huu unaoletwa duniani na zaidi anatutambua sisi wanadamu katika udhaifu wetu. Pengine udhaifu wa kukata tamaa mapema, au kupenda zaidi mali, vyeo, madaraka na pesa. Kristo anatutaadharisha kwamba “angalieni”. Tambueni nguvu mlizo nazo kama Kondoo na hivyo mbele ya mbwa-mwitu mnahitaji nguvu za ziada. Pia anawaambaia kuwa mbele ya mbwa-mwitu ni ujasiri tu wa kipekee unahitajika kusudi kuweza kusonga mbele. Hapa inadokezwa nafasi ya msaada wa kimungu ambao ni neema zake zitakazotupatia ujasiri wa kusonga mbele na kuutimiza utume huu. Hivyo agizo hili “angalieni” ni wito wa kubaki tumeungana na Mungu katika Neno lake, Sala na Sakramenti. Tukio hili la Kondoo kupambana na mbwa-mwitu si la kawaida lakini kwa uwezo wa Mungu tutashinda.

Ujumbe tunaotumwa kuutangaza ni amani. “Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza Amani iwemo nyumbani humu”. Amani wanayotumwa kuitangaza ni amani ya Kristo Mfufuka. Amani hiyo si kama ile ya ulimwengu ambayo imejikita katika vitu, madaraka na umaarufu wa kibinadamu bali ni amani ile ya kuwa na Mungu ndani mwako. Amani tunayopewa na Kristo inaambatana na Upendo na huruma yake. Ni amani ambayo inatupatanisha tena na Mungu na mwanadamu mwenzetu na hivyo kutufanya kuishi kindugu kweli kweli bila kujali kupata kitu kuzidi wengine. Ni amani ambayo daima inanuia mema kwa wengine. Hiyo ndiyo amani inayoletwa na Kristo na ambayo tunatumwa kwenda kuitangaza, na hiyo ndiyo amani ambayo mwanadamu katika hali ya dhambi ameipoteza na yupo katika hamu kubwa ya kuwa na amani hiyo.

Uthabiti katika mafundisho ni muhimu sana kwa sisi kama wanakanisa katika kuutekeleza utume wetu. “Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii”. Pale mtume wa Kristo anaposhindwa kueleweka kama kweli yeye ni wa moto au wa baridi hapo ndipo anapoteza sifa ya kuwa mtumishi mwaminifu. Hatupaswi kuwa kama bendera inayofuta upepo. Leo hii unasema hili na kesho unatenda hili. Hili ni onyo la kuepa kufanya utume kwa ajili kuwafurahisha wale unaowatumikia. Mara nyingi sisi kama wanakanisa huingia katika vishawishi vya kutaka kusawazisha mapokeo au mazoea mahalia na Injili ya Kristo kwa kusudi tu na kuepuka mafarakano nao. Injili tunayoitangaza inakosa nguvu kwani leo tunaipambanua katika namna hii na kesho kwa namna ile. Namna hii ya utumishi haitatupatia ufanisi wa kweli.

Mwisho Injili ya leo inatutaka kushirikiana na tunaowahudumia katika maisha yao ya kila siku. “Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapoozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umekaribia”. Hii inaunganika vizuri na tunaloambiwa katika somo la kwanza la leo, juu ya Yerusalemu mpya ambayo ni sababu ya furaha kwa wote. Kanisa linakuwa kama Yerusalemu mpya pale tu linapoingia katika maisha ya kawaida ya mwanadamu na kumgusa katika maisha yake ya kawaida kwa kumfunulia ufalme wa mbinguni. Ndiyo hiyo habari njema ambayo wanahitaji kuisikia wanadamu na kwa habari hiyo kweli watapata kufurahi na kushangilia, kunyonya na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake na kukama na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake.

Somo hilo la kwanza linatuwekea taswira mbalimbali ambazo zinapaswa kuambatana na utume wetu. Moja ya taswira hiyo ni “mfano wa mama anayefariji mtoto wake juu ya magoti yake”. Hivyo utangazaji wetu wa ufalme wa Mungu katikati ya jamii ya mwanadamu inapaswa kujikita katika kuwaganga wagonjwa wa kiroho na kimwili, kuwafungua waliofungwa na kongwa la utumwa wa shetani na kuwaangazia wale ambao wapo katika giza na wamepoteza kabisa matumaini. Tuingie nyumbani mwao na kula vinavyowekwa mbele yetu, yaani tupokee hayo machungu yao na kuyahisi sawasawa ndani mwetu na kisha tuwasadie kuwatoa huko na hilo ndilo tangazo letu kwao ya kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.

Mtume Paulo katika somo la pili anatupatia msingi ambao ni Msalaba wa Kristo. “Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu unasulubiwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu”. Watakatifu wengi walichota nguvu zao za kuutekeleza utume wao kupitia juhudi zao za kujiunganisha na msalaba wa Kristo. Padre Pio aliwahi kusema maneno haya juu ya msalaba: “Jambo hili nimelitamani kwa moyo wangu wote, kuujua, kuupenda na kuuishi msalaba. Kwa maana katika msalaba kuna wokovu”. Kadiri ya mafundisho ya Mtakatifu Thomaso wa Akwino tunaambiwa kwamba katika msalaba tunajifunza fadhila za unyenyekevu, utii, uvumilivu, msamaha, ujasiri na katika ujumla wake upendo. Ni kwa njia ya faadhila hizi ndipo tunaweza kupata ujasiri wa kutoka kama Kondoo na kupita kati ya mbwa-mwitu na kuwatangazia watu kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.

Tuombe neema ya Mungu katika Dominika hii kusudi kwa msaada wake tuweze kweli kuwa mawe hai ya kuijenga Yerusalemu mpya, yaani Kanisa, na hivyo kuutangaza Ufalme wake kwa watu wote.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.