2016-06-29 11:02:00

Papa awakumbuka waliokumbwa na shambulizi la kigaidi Uturuki!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 29 Juni 2016 amewakumbuka na kuwaombea watu 36 waliofariki dunia na wengine 140 kujeruhiwa vibaya kutokana na shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ataturk, huko Istanbul, nchini Uturuki, siku ya Jumanne, tarehe 28 Juni 2016. Baba Mtakatifu anasema anaendelea kusali na kuwaombea wale wote walioguswa na msiba huu mzito. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa watu hawa wenye mioyo ya shari na kusaidia kuwaongoza watu kwenye njia ya amani.

Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni kumehitimishwa Mkutano wa Kimataifa kuhusu Uwekezaji unaowajibisha ili kupata mafao ya kijamii; mkutano ambao ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “Kuufanya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uwe mwaka wenye mafao kwa maskini”. Baba Mtakatifu anaombea ili kweli mchakato wa uwekezaji kutoka katika sekta binafsi kwa kuunganisha na nguvu za uwekezaji wa serikali, usaidie katika mapambano dhidi ya umaskini kwa watu wengi wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa makundi makubwa ya majuhaji kutoka ndani na nje ya Italia, akawatakia wote heri na baraka tele katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba wa imani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka waamini wa Jimbo kuu la Roma wanaoadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, wasimamizi wao. Anawatakia baraka wote wanaoendelea kujibidisha katika matendo ya huruma kwa ajili ya kuchangia huduma ya upendo huko Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.