2016-06-27 14:52:00

Papa Francisko akabidhi matunda ya hija yake Armenia kwa B. Maria


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 26 Juni 2016 amehitimisha hija yake ya kitume nchini Armenia. Kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa “Zvartnots” mjini Yerevan, akiwa ameandamana na Patriaki Karekin II walipokewa na Rais wa Armenia na baada ya mazungumzo ya faragha kati ya viongozi hawa wawili, nyimbo za mataifa haya mawili zilipigwa, baadaye Baba Mtakatifu akaagana na wenyeji wake na kuanza safari ya kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake.

Akiwa njiani alipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake na kujibu maswali kumi ya nguvu. Alipowasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ciampino, mjini Roma, majira ya saa 1:30 za Usiku kwa saa za Ulaya, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu ili kutoa shukrani zake za dhati kwa Bikira Maria kwa kumwezesha kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Armenia pamoja na kumkabidhi matunda ya safari hii ya kitume yatakayoonekana kwa wakati wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.