2016-06-27 06:39:00

Makanisa yashikamane ili kushuhudia tunu msingi za Kikristo!


Patriaki Karekin II wa Kanisa la Kitume la Armenia, Jumapili tarehe 26 Juni 2016 ameongoza Liturujia Takatifu ambamo Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki kikamilifu. Sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza tafakari yake ni pale ambapo Yesu aliwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake baada ya kuwaonea huruma kwa kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu na kuwaponya magonjwa yao.

Sehemu hii ya Injili ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo linalohamasishwa kuonesha huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuendelea kupyaisha imani kwa njia ya matendo ya huruma yanayodhihirisha moyo wa sala, kielelezo cha mwanadamu kuendelea kushiriki katika kazi ya uumbaji. Kwa njia ya mwono huu, Kanisa limeweza kupata mashuhuda wengi wa imani, walioandika kurasa za maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya mahubiri yao, lakini zaidi kwa njia ya matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji na uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Leo hii mwanadamu anakabiliwa na changamoto nyingi za maisha kama vile: Sera na siasa potofu; misimamo mikali ya kidini na kiimani; ubaguzi na nyanyaso za kila aina; matumizi haramu ya dawa za kulevya; ubinafsi, uchoyo na uchu wa mali. Kuna ukanimungu pamoja na kusambaratika kwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kifamilia. Kwa bahati mbaya mwanadamu anataka kujenga dunia pasi na uwepo wa Mungu wala Amri na maagizo yake, matokeo yake ni sera tenge za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazopelekea uharibifu wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusambaratisha uhalisia wa maisha ya binadamu.

Patriaki Karekin II anakaza kusema, pamoja na mambo yote haya, lakini ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kumwangalia mwanadamu kwa jicho la huruma, mapendo na tunza yake, ataendelea kuwaenzi wale wote waliopondeka moyo na kuwaimarisha wasiokuwa na imani na matumaini. Atakuwa ni chemchemi ya faraja kwa wagonjwa na wenye huzuni na kwamba, iko siku Amri za Mungu na kanuni maadili vitaweza tena kutawala katika maisha ya binadamu. Kanisa linapaswa kuendeleza utume huu.

Patriaki Karekin II anasema Kanisa linapaswa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo; kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kushikamana kwa dhati kupambana na changamoto mamboleo. Kanisa liendelee kuonesha mshikamano wa dhati na wale wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma za kidini, ili waweze kupata maendeleo endelevu, amani na utulivu viweze tena kutawala kati yao. Anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kusimama kidete kutetea maskini na wanyonge, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; amani, ustawi na mafao ya wengi. Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuyaimarisha Makanisa haya katika imani na mapendo, ili yaendelee kushirikiana na kushuhudia umoja na udugu; upendo na mshikamano na waathirika wa vita pamoja na vitendo vya kigaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.