2016-06-27 07:30:00

Armenia inapaswa kujikita katika mchakato wa majadiliano na amani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 26 Juni 2016 amehitimisha hija yake ya kitume nchini Armenia iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “kutembelea nchi ya kwanza ya Kikristo”. Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu alipata bahati ya kuwaandikia Marais na wakuu wa nchi ambazo alipitia wakati akiwa angani ili kuwatakia heri, baraka na matashi mema. Baba Mtakatifu amewaandikia ujumbe wakuu wa nchi ya Armenia, Uturuki, Bulgaria, Serbia, Montenegro, Bosnia- Erzegovina, Croazia na Italia.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawashukuru wananchi wa Armenia kwa mapokezi yao makubwa na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini humo. Anawatakia wote: baraka, amani na ustawi. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema anarejea kutoka katika hija yake ya kitume nchini Armenia, ambako amepata nafasi ya kukutana na familia ya Mungu ili kuwaonjesha upendo wake pamoja na kumshukuru Mungu kwa utajiri mkubwa wa historia unaofumbatwa na Jumuiya za Kikristo nchini humo.

Ameiomba familia ya Mungu nchini Armenia kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano na amani. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Rais Mattarella pamoja na wananchi wote wa Italia, daima akijitahidi kukoleza mchakato wa ukuaji wa uchumi pamoja na kusikiliza kilio na mahitaji ya wananchi wake hususan familia msingi wa mafungamano na maendeleo ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.