2016-06-25 08:46:00

Ujumbe kwa siku ya utalii duniani kwa mwaka 2016


Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 27 Septemba 2016 itaadhimisha Siku ya Utalii Duniani ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Utalii kwa wote- wote wawezeshwe”. Huu ni ujumbe ambao umetolewa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, ambao unakazia pamoja na mambo mengine utalii unaowakumbatia wengi; utalii ambao watu wengi zaidi wanaweza kufaidika nao; utalii endelevu ambao unajenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii.

Huu ni utalii ambao unaotoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na watu wasiokuwa na uwezo, kama kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kimsingi hii ni Siku ya Kimataifa ambayo pia Vatican inashiriki kikamilifu kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na sekta ya utalii katika mchakato wa ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa watu. Ni sekta yenye changamoto na fursa ambazo zikitumiwa vyema zinaweza kuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya watu wanaojipatia nafasi ya mapumziko na kwenda kuvinjari sehemu mbali mbali za dunia imeongezeka maradufu. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2015 zinaonesha kwamba, idadi ya watalii imeongezeka hadi kufikia watalii millioni moja, laki moja na themanini na nne elfu. Idadi ya watalii wa kimataifa inakadiriwa kufikia billioni mbili ifikapo mwaka 2030.

Ongezeko hili la watalii duniani linaendelea pia kutoa mwelekeo chanya wa utalii wa kimataifa katika medani mbali mbali za maisha, bila kusahau kwamba, utalii huu pia kwa miaka mingi umekuwa unabeba mapungufu makubwa katika undani wake. Hapa kuna haja kwa sekta ya utalii kufanya maboresho makubwa katika mwelekeo wake, ili kweli uweze kufumbatwa na ubinadamu; utalii iwe ni fursa ya mapumziko, wakati wa kujiongezea ujuzi na maarifa; kugundua na kuthamini tamaduni, mila na desturi za watu wa mataifa na kwamba, utalii ni chombo cha kukuza mchakato wa uchumi na maendeleo ya watu.

Sekta ya utalii ni chachu ya amani na majadiliano; fursa ya elimu na ukuaji wa mtu binafsi; mahali pa binadamu kukutana na mazingira, nyumba ya wote sanjari na kukua kiroho. Kutokana na mwelekeo kama huu, hapa inawezekana kusema kwamba, utalii ni haki ambayo inampatia mtu nafasi ya kujipumzisha na kujistarehesha, ili kujichotea nguvu ya kuendelea mbele na mapambano ya changamoto za kila siku. Haki hii inatambuliwa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu kadiri ya Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililochapishwa kunako mwaka 1948.

Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, haki hii msingi si kwa kila mtu, kuna watu wengi ambao bado hawajatendewa haki hii kutokana na sababu mbali mbali. Hii ni changamoto si tu kwa ajili ya nchi zinazoendelea duniani bali hata kwa nchi zilizoendelea zaidi. Bado watu wengi wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi kiasi kwamba, hawana uwezo wa kugharimia utalii, ndiyo maana kwa sasa kuna kampeni ya kimataifa ili kuhakikisha kwamba, utalii unawahusisha watu wengi zaidi bila kuwasahau hata walemavu.

Hapa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum linakazia umuhimu wa utalii kuwa ni kwa ajili ya wote, endelevu, kijamii na ushuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini. Mchakato wa utalii unapaswa kuwa ni sehemu ya huduma kwa ajili ya utimilifu wa binadamu sanjari na maendeleo endelevu ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.