2016-06-25 07:35:00

Uingereza yafanya maamuzi magumu na athari zake zaanza kuonekana!


Wananchi asilimia 52% wa Uingereza walioshiriki kwenye kura ya maoni wamefanya maamuzi mazito kwa kupiga kura ya maoni ambayo imewaengua kutoka katika Umoja wa Ulaya hali ambayo imepelekea hata Waziri mkuu wa Uingereza Bwana David Cameron kubwaga manyanga na kuwasilisha hati rasmi kwa Malkia wa Uingereza. Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2016. Maamuzi haya machungu yamepokewa na Jumuiya ya Kimataifa kwa hisia tofauti.

Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles anasema, Uingereza imeandika ukurasa mpya wa maisha na utume wake katika Jumuiya ya Kimataifa, historia ambayo itakuwa na athari kubwa katika medani za kisiasa, kiuchumi na mafungamano na Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi hiki ni kipindi kigumu kwa wananchi wote wa Uingereza kwani hatima yao kwa sasa haijulikani sawa sawa.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki kwamba, Serikali na viongozi wa kisiasa wataheshimu maamuzi ya wananchi wa Uingereza, licha ya maoni tofauti yaliyojitokeza nchini humo. Hapa maskini na watu wasiokuwa na sauti wanapaswa kulindwa na Serikali, ili watu wengi wasijikute wakikosa fursa za ajira pasi na sababu msingi wala wanchi wengine kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu kutokana na ugumu wa maisha utakaojitokeza baada ya kura hii ya maoni.

Kardinali Nichols anasema, Uingereza ni nchi ambayo imekuwa na utamaduni wa ushirikiano wa kimataifa ni matumaini ya Kanisa kwamba, Uingereza itaendeleza utamaduni wa ukarimu, ukweli na uwazi, kwa kuwapokea na kuwakirimu watu wanaohitaji msaada zaidi. Hapa wananchi wote wa Uingereza wanapaswa kushikamana kwa dhati, ili kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi yao bila kusahau mafao ya wengi duniani.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Justin Welby anawataka wananchi wa Uingereza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na wala si kuta zinazowatenganisha watu. Waingereza washikamane kwa dhati kabisa katika mchakato wa ujenzi wa nchi inayojikita katika moyo wa ukarimu na mapendo na kwamba, sasa wanapaswa kujifunga kibwebwe ili kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazoibuka baada kura ya maoni ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Hapa wananchi watambue kwamba, wanawajibika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi yao; waguswe na mahangaiko ya watu kutoka nchi mbali mbali waliokuwa wanaishi nchini Uingereza kutoka katika nchi za Umoja wa Ulaya. Katika kipindi hiki kigumu cha historia ya Uingereza, wananchi wanapaswa kujikita katika kanuni ya: Umoja, matumaini na ukarimu ili kuweza kukivuka kipindi hiki kigumu cha mpito kuelekea uhuru kamili wa wananchi wa Uingereza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.