2016-06-25 14:09:00

SECAM: Kumekucha huko Luanda, Angola!


Maandalizi ya Mkutano wa 17 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, utakaoadhimishwa huko Luanda, Angola, kuanzia tarehe 18 Julai hadi tarehe 25 yanaendelea kwa kasi kubwa. Zaidi ya wajumbe 100 wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi za SECAM wanatarajiwa kushiriki kikamilifu, bila kuwasahau wadau na wafadhili kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ili kufanikisha mahudhurio ya mkutano huu, Serikali ya Angola imeamua kutoa vibali maalum kwa wajumbe wa mkutano huu.

Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Familia Barani Afrika, Jana, Leo na Kesho: kadiri ya Mwanga wa Injili” Hii itakuwa ni fursa kwa Kanisa Barani Afrika kupembua kwa kina na mapana changamoto za maisha na utume wa familia kadiri ya mazingira ya Bara la Afrika baada ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, Katekesi ya kina ya Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, Wosia wa Kitume, “Furaha ya upendo ndani ya familia kuchapishwa hivi karibuni kama dira na mwongozo wa utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Kamati tendaji ya SECAM chini ya uongozi wa Askofu mkuu Gabrieli Mbilingi wa Jimbo kuu la Lubango, itaanza kikao chake tarehe 18 Julai 2016, kwa Ibada ya Misa takatifu itakayoadhimishwa kwenye Parokia ya Familia Takatifu, Jimbo kuu la Luanda, Angola. Ataongoza na kutoa hotuba elekezi ya mkutano wa SECAM kwa siku ya kwanza pamoja na kusikiliza ujumbe na matashi mema kutoka kwa wadau mbali mbali.

Mkutano huu utakuwa ni fursa kwa Kanisa Barani Afrika kupembua kwa kina na mapana changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa famila ndani ya Bara Afrika. Lengo ni kuendelea kuimarisha  utume wa familia Barani Afrika, ili kweli familia ya Mungu Barani Afrika iwe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia. Wajumbe wa SECAM watapitia kwa mara nyingine tena utekelezaji wa maamuzi yaliyopitishwa na SECAM kwenye mkutano wake 16 ulioadhimishwa mwezi Julai, 2013 nchini DRC. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar pamoja na taasisi zake, zitatoa taarifa rasmi wakati wa mkutano huu.

Ratiba inaaonesha kwamba, tarehe 23 Julai 2016, itakuwa ni siku ya kutangaza mahali na tema itakayoongoza mkutano wa 18 wa SECAM, hususan wakati huu, SECAM inapojiandaa pia kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1969 wakati wa hija ya kitume ya Mwenyeheri Paulo VI nchini Uganda. Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya SECAM ni hapo mwaka 2019. Baadhi ya wajumbe wa SECAM, tarehe 24 na 25 Julai 2016 watapata nafasi ya kumtembelea Rais wa Angola. Mkutano wa 17 wa SECAM utafungwa rasmi hapo tarehe 24 Julai 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.