2016-06-25 09:45:00

Prof. Roger Houngbèdji ateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Cotonou, Benin


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Antoine Ganyè wa Jimbo kuu la Cotonou, Benin la kung’atuka kutoka madarakani kwa mujibu wa Sheria za Kanisa namba 401§ 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Roger Houngbèdji kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo kuu la Cotonou, Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Jaalim wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Magharibi, (UCAO) na Taasisi ya Wadomenikani ya Mtakatifu Tomma wa Akwino, mjini Yamoussoukro.

Askofu mteule Roger Houngbèdji alizaliwa tarehe 14 Mei 1963. Kunako mwaka 1984 akajiunga na Shirika la Wadominikani na kuweka nadhiri zake za daima kunako mwaka 1989. Baada ya majiundo ya kitawa na kipadre, akapewa Daraja Takatifu hapo tarehe 8 Agosti 1992. Tangu wakati huo, amejikuta sehemu kubwa ya maisha na utume wake akiwa katika malezi huko Pwani ya Pembe na Cameroon.

Pole pole alianza kuingia katika masuala ya uongozi wa Shirika tangu mwaka 1997 – 2007 kama Mwakilishi wa mkuu wa Vikarieti ya Afrika Magharibi na hatimaye kama Mkuu wa Kanda ya Afrika Magharibi kwa vipindi viwili, yaani tangu mwaka 2009 – 20015. Askofu mteule Roger Houngbèdji  ni Jaalim na kwa awamu mbili alichaguliwa kuwa ni Rais wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa nchini Pwani ya Pembe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.