2016-06-24 07:20:00

Familia ni mdau mkuu wa maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili!


Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ni matunda ya tafakari ya kina iliyofanywa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi ambayo ilimwilishwa katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi zake za Jumatano kwa kipindi cha mwaka mzima. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Kuna uhusiano wa karibu kati ya tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu “Kanisa katika ulimwengu mamboleo”, “Gaudium et spes”; Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” pamoja na Waraka wa kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” “Laudato si” bila kusahau nyaraka nyingine muhimu ambazo zimetolewa na viongozi wa kuu wa Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Kanisa linapenda kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango na ukuu wa Mungu kwa kutambua kwamba, hakuna familia ambayo imekamilika, lakini kila familia inapaswa kuwa ni sehemu ya mchakato kuelekea ukomavu na utakatifu wa maisha. Kanisa linatambua fika changamoto na vikwazo vinavyoendelea kutikisa misingi ya maisha na utume wa familia kwa kukumbatia utamaduni wa kifo! Haya yamesemwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia, siku ya Alhamisi, tarehe 23 Juni 2016 wakati wa uzinduzi wa Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva.

Kanisa kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa za maisha na utume wa familia katika ulimwengu na Kanisa katika ujumla wake, likaamua kujitaabisha ili kufanya tafakari ya kina kwa ajili ya kulinda, kudumisha na kuendeleza Injili ya familia, kwa kuzilinda na kuzisaidia familia zinazoogelea katika shida na magumu; familia ambazo zina majeraha na makovu ya kinzani na utengano; ili familia zote hizi ziweze kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Lengo ni kukuza ushuhuda, umoja na mshikamano; kusimama kidete kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji, kanuni maadili na utu wema; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi;mambo yanayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji! Wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” unafafanua kwa kina na mapana dhana ya familia kadiri ya Maandiko Matakatifu kwa kuonesha upendo wa dhati na changamoto zake kama vile: wakimbizi na wahamiaji; dhana ya usawa wa kijinsia; utamaduni wa kifo unaokumbatiwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba; ukosefu wa fursa za ajira; nyanyaso za kijinsia; kipigo kwa wanawake; walemavu pamoja na upweke hasi inaotishia amani, usalama na utulivu wa watu ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu katika Wosia huu wa kitume anafafanua wito wa familia mintarafu Mafundisho ya Yesu Kristo yalivyofafanuliwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa kukazia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa inayojikita katika udumifu, mapendo kamili, uaminifu na dhamana ya malezi kwa watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuzisaidia familia kwa kuzingatia hali halisi na wala si “familia za kuchongwa”. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa familia hazina budi kujikita katika: Mafundisho tanzu ya Kanisa; kanuni maadili na utu wema pamoja na kutumainia neema na huruma ya Mungu katika maisha ya binadamu.

Askofu mkuu Paglia anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu anakazia Injili ya familia inayojikita katika upendo kamili kati ya Bwana na Bibi kama anavyosimulia Mtakatifu Paulo katika utenzi wake juu ya upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu asili na wema na utakatifu wote. Familia hazina budi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbata zawadi ya maisha na mafungamano ya kijamii bila kusahau changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa elimu na malezi kwa watoto ndani ya familia na jamii katika ujumla wake pamoja na kuwa na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji yatakayozisaidia familia kutekeleza dhamana na wajibu wake mkamilifu. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuzisindikiza familia; kuwa na mang’amuzi na hatimaye, kuzishirikisha katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwongozo wa jumla kwa ajili ya utume wa familia.

Askofu mkuu Paglia anasema, Familia ina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu changamoto ni kuheshimu utofauti unaojitokeza kati ya bwana na bibi na kwamba, jinsia hizi mbili zinahitajiana na kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu; tayari kushiriki katika kazi ya uumbaji na kuwajibika barabara katika malezi na makuzi ya watoto wao ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutunga sera zitakazosaidia mchakato wa maboresho ya familia kwa kuwa na fursa za ajira ili kuchangia katika ustawi na maendeleo: kiuchumi na kijamii ili hatimaye, kuondokana na mambo ambayo yanaweza kuzitumbukiza familia katika mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Familia ziwezeshwe kuchangia katika haki na maani kwa kujikita katika mshikamano wa umoja, upendo na udugu. Familia ni shule ya huruma na mapendo, mahali ambapo watu wanaweza kumwilisha ndoto bora za maisha yao.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anahitimisha kwa kusema, haya ndiyo mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuishirikisha Jumuiya ya Kimataifa katika Wosia wake wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ili familia ziweze kupeta katika maendeleo ya kiroho na kimwili ili haki na amani viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.