2016-06-22 09:01:00

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ya kimaadili na kijamii!


Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa kichungaji “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” “ Laudato si” juu utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini, magonjwa, vita na kinzani za kijamii, ili hatimaye kujenga na kudumisha furaha, amani na utulivu. Uharibifu wa mazingira unahitaji wongofu wa kiekolojia unaobadili mfumo mzima wa maisha ya binadamu kwani hii ni dhamana ya kijamii sanjari na matumizi bora zaidi ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu kuchapishwa kwa waraka huu wa kitume hapo tarehe 18 Juni 2015 anasema, Baraza lake limeanzisha tovuti mpya inayopembua kwa kina na mapana Waraka huu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa anuani ifuatayo: www.laudatosi.va. Tovuti hii inafafanua kwa kina jinsi ambavyo waraka huu umesambazwa na kupokelewa kwa mikono miwili ndani na nje ya Kanisa, kwani unatoa mifano bora na hai ya jinsi ya kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Turkson ameyasema haya Jumatatu tarehe 20 Juni 2016 kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Montesanto lililoko mjini Roma, wakati wa kongamano lililoandaliwa kwa ajili ya kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu kuchapishwa kwa waraka huu wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waraka huu katika tovuti hiyo umeandikwa kwa lugha tano yaani: Kiingereza, Kiitalia, Kifaransa, Kireno na Kihispania. Watumiaji wa mtandao huu wanaweza pia kushirikisha maoni yao pamoja na kusoma machapisho ya makongomano mbali mbali mintarafu waraka huu.

Kwa upande wake Padre Walter Insero, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Jimbo kuu la Roma anasema, Waraka wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unaweza kumwilishwa kikamilifu zaidi wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kuwa na mwelekeo wa maisha ya kiroho yanayokazia: mwelekeo wa kitaalimungu kuhusu ekolojia, maisha ya kiroho mintarafu ekolojia na umuhimu wa kiekumene unaofumbatwa katika Waraka huu, kama ulivyopembuliwa na Mwakilishi wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli wakati wa uzinduzi wa Waraka wa Laudato si.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Lesvos pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni kielelezo na changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote dhidi ya uharibifu wa mazingira, ukosefu wa amani na utulivu unaopelekea uwepo wa makundi makubwa ya wahamiaji duniani. Utu na heshima ya binadamu viko rehani kutokana na uchafuzi na uharibu wa mazingira unaofanywa na binadamu. Hapa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa ni watunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii pia ni dhamana ya kimaadili inayopaswa kutekelezwa na viongozi wa Jumuiya Kimataifa, changamoto ambayo imekuja kwa wakati kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wake wa kitume, “Laudato si” yaani“Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.