2016-06-22 15:39:00

Tema ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, 2017


Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti! Hii ndiyo kauli mbiu ambayo imechaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wahamiaji na wakimbizi  Duniani itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 15 Januari 2017. Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi linasema, wakimbizi na wahamiaji ni dhana ya kawaida katika historia na maisha ya binadamu na wala si jambo linalojitokeza Barani Ulaya au kwenye Bahari ya Mediterrania.

Mabara yote yanaguswa na kutikiswa na dhana ya wakimbizi na wahamiaji na hawa si wale watu wanaotafuta fursa za ajira au hali bora zaidi ya maisha, lakini pia kuna watu wazima na watoto wanaokimbia hali ngumu ya maisha na majanga asilia! Ni jambo la msingi kuhakikisha kwamba, katika kila nchi ambamo wanapokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na familia zao, wawe na nafasi ya kufurahia haki zao msingi kama wakimbizi na wahamiaji. Hii ndiyo hali ambayo inatia wasi wasi mkubwa kwa watoto wanaojikuta wakiwa uhamishoni kama wakimbizi na wahamiaji katika uwanja wa kimataifa.

Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum linakaza kusema watoto na wanawake ni waathirika wakubwa katika wimbi hili kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wakati mwingine hawaonekani kwani hawana vibali wala nyaraka za kusafiria. ”Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti” ni kauli mbiu ambayo Baba Mtakatifu anapenda Kanisa liweze kuifanyia kazi kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao wanajikuta wakiwa ni wahamiaji au wakimbizi bila ya kuwa na ulinzi au usimamizi kutoka kwa wazazi na walezi wao.

Hili ni kundi ambalo sauti yake inapaswa kusikilizwa kwa makini. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu atachapisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku hii. Maadhimisho haya kwa mwaka 2017 yanapata chimbuko lake kutoka katika barua iliyoandikwa na Baraza la Kipapa kunako tarehe 6 Desemba 1914 inayojulikana kama ”Uchungu na wasi wasi””Il dolore e le preoccupazioni” na kutumwa kwa Maaskofu Katoliki nchini Italia.

Kwa njia ya barua hii, Kanisa liliwataka Maaskofu Katoliki kuwa na siku maalum ambayo ingesaidia mchakato wa uragibishaji wa mateso na mahangaiko ya wahamiaji pamoja na kuchanga fedha kwa ajili ya kugharimia mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Waitaliani waliokuwa wameikimbia nchi yao sanjari na kutoa majiundo makini kwa Wamissionari ambao wangejisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wahamiaji. Kutokana na wito huu, kunako tarehe 21 Februari 1915, kwa mara ya kwanza Kanisa likaadhimisha Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.