2016-06-21 07:59:00

Bila haki, amani na utulivu hakuna maendeleo ya kweli!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika tamko lake linapongeza juhudi za serikali ya Nigeria katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kutikisa: Umoja, usalama, uchumi, maadili, utu wema, rushwa na ufisadi. Maaskofu wanaitaka familia ya Mungu nchini Nigeria kujifunga kibwebwe ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi nchini Nigeria.

Taifa linahitaji kwa namna ya pekee kujikita katika utawala bora unaozingatia na kuheshimu sheria, ili kweli: haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi yaweze kufikiwa. Bila tunu hizi msingi sera na mikakati ya ustawi na maendeleo ya nchi vitakwama. Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa nchini Nigeria yanakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, kiasi kwamba, wananchi wanakosa imani na serikali yao. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa ya kitaifa inayopaswa kufanyiwa kazi, vinginevyo, wanasiasa uchwara wanaweza kuwatumia vijana hawa kwa ajili ya kuvuruga amani na utulivu nchini Nigeria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaitaka Serikali kusimama kidete kulinda maisha na mali za wananchi wa Nigeria kwani hii ni dhamana yake ya kwanza. Familia ya Mungu nchini Nigeria katika ujumla wake, inahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ulinzi na usalama kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Ili kufikia azma hii, kuna haja ya kuwa na toba na wongofu wa ndani, unaotoa mwelekeo mpya wa maisha kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao msingi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linawaahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi nchini Nigeria. Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, licha ya changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo kwa sasa.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu ataweza kusikiliza sauti na kilio cha watu wake na hivyo kuwajalia tena amani na utulivu; ustawi na maendeleo ya kweli: kiroho na kimwili. Waamini wawe mstari wa mbele katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, wanahitimisha Maaskofu katika tamko lao ambalo limetiwa mkwaju na Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria pamoja na Askofu William Avenya, Katibu mkuu, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.