2016-06-20 07:25:00

SECAM: hatima ya Burundi iko mikononi mwa wananchi wenyewe!


Ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagasca, SECAM umehitimisha hija ya amani, udugu na mshikamano kwa kutembelea familia ya Mungu nchini Burundi ambayo kwa sasa inaogelea katika kinzani na mipasuko ya kisiasa na kijamii, hali iliyojitokeza tangu mwezi Mei, 2015 baada ya Rais Pier Nkurunziza kuamua tena kuwania madaraka katika awamu ya tatu, kinyume kabisa cha Katiba ya nchi na Mkataba wa amani ulitiwa sahihi mjini Arusha, Tanzania.

Katika kinzani hizi, kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha yao, makundi makubwa ya watu wanakimbia Burundi ili kutafuta usalama wa maisha na wengine hawana makazi ya kudumu hata ndani ya Burundi yenyewe. Umoja wa Mataifa unachelea kusema, kama Jumuiya ya Kimataifa haitachukua hatua madhubuti, Burundi inaweza kutumbukia tena katika mauaji ya kimbari!

Wajumbe wa SECAM wanakaza kusema hatima ya maisha, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Burundi iko mikononi mwao wenyewe. Inasikitisha kuona kwamba, hivi karibuni, Barani Afrika kumeibuka siasa zenye ukinzani kiasi hata cha kupandikiza utamaduni wa kifo, nyanyaso na dhuluma, kiasi hata cha kuhatarisha mafungamano ya kijamii Barani Afrika kwani kuteteteleka kwa amani nchini Burundi ni hatari kwa amani kwa nchi jirani na Burundi.

Katika tamko lao, Ujumbe wa SECAM uliokuwa chini ya Askofu Sithembele Anthon Sipuka wa Jimbo Katoliki Umtata, Afrika ya Kusini, wanawashukuru Maaskofu Katoliki nchini Burundi, kwa kuwaonesha ukarimu na hivyo kugundua kiu ya amani na utulivu; ustawi na maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wanaishukuru Serikali ya Burundi kwa kuwazesha kushiriki katika mchakato unaopania kukoleza majadiliano ya kweli na uwazi, ili amani ya kudumu iweze kupatikana nchini Burundi, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

SECAM inatambua shida na mahangaiko ya wananchi wa Burundi pamoja na jitihada za Jumuiya Kimataifa za kutaka kuhakikisha kwamba, amani ya kweli inapatikana nchini Burundi. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni njia muafaka katika kutatua mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Burundi: Amani na utulivu ni mambo msingi yanayopaswa kuendelezwa kwa kujikita katika mchakato wa msamaha, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa.

Kanisa Barani Afrika litaendelea kuonesha mshikamano wa hali na mali na katika sala, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini Burundi kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano kati ya Serikali ya Burundi na vyama vya upinzani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kuwekeza katika mchakato wa majadiliano, ili kweli amani iweze kurejea tena nchini Burundi, bila kuingiliwa na mataifa mengine katika mambo yake ya ndani. SECAM inalaani kwa nguvu zote biashara haramu ya silaha inayofanywa nchini Burundi na hivyo kuendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya wanapaswa kusaidia jitihada za kusitisha biashara ya silaha Barani Afrika kwani inaendelea kukwamisha ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika katika ujumla wake.

Ujumbe wa SECAM unahitisha tamko lake kwa kusema, Familia ya Mungu Barani Afrika itaendelea kusali kwa ajili ya kuombea utulivu na amani; ustawi na maendeleo ya wananchi wa Burundi katika ujumla wao. Watambue kwamba, mustakabali wa nchi yao uko mikononi mwao wenyewe na kwamba, SECAM itaendelea kuwatia shime kwani wote ni wamoja katika Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.