2016-06-20 07:11:00

Hata walemavu wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, Jumapili tarehe 19 Juni 2016 limeadhimisha Siku ya Uhai Kitaifa na kwamba, wale wote walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya wamepata baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili waweze kudumu katika nia hii njema ya kuwa ni mashuhuda na watetezi wa Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na kuwajali watu wenye ulemavu. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa nchini Uingereza imekuwa ni fursa ya kutafakari na kushangaa zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hiki ni kielelezo kikubwa cha kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza. Maadhimisho ya mwaka huu yamewaangalia kwa jicho la upendo walemavu ambao wanapaswa kuthaminiwa, kupendwa na kuhudumiwa kwa moyo wote kama inavyofanya Jumuiya  L’Arche iliyoko nchini Ufaransa, iliyoasisiwa  na Jean Vanier. Hapa ni mahali ambapo watu wenye ulemavu wanajisikia kuheshimiwa, kupendwa na kuthaminiwa jinsi walivyo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles linasema, hapa binadamu anapaswa kusimama na kufanya tafakari ya kina ili kushangaa juu ya zawadi ya uhai ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu. Watu wanyenyekevu na wenye moyo mnyofu ndio wanaoweza kupata mshangao wa zawadi ya uhai, lakini wengine wanaweza kuona ni jambo la kawaida tu. Inawezekana baadhi ya watu kuwabeza walemavu kutokana na hali yao, kumbe hapa mwanadamu anahimizwa kuthamini zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.