2016-06-20 10:30:00

Familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya!


Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika maisha na utume wa familia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima; ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai, huruma na mapendo. Familia za Kikristo hazina budi kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya vikwazo na kinzani zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Kanisa linatambua dhamana, wito na utume wa familia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa na katika jamii katika ujumla wake. Kumbe, familia zinapaswa kuwa kweli ni kitovu cha Uinjilishaji mpya kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Kwa namna ya pekee, familia zinahamasishwa kuwa ni hule ya utu wema; haki na amani; huruma, samaha na mapendo ili kuweza kupambana na vikwazo pamoja na vizingiti vinavyojitokeza katika maisha na utume wake, ili kamwe familia zisijekumezwa na malimwengu pamoja na ukanimungu unaojitokeza kwa kasi kubwa kwenye ulimwengu mamboleo.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia anakaza kusema, familia nyingi zinashindwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji mpya kutokana na mazingira magumu zinazokumbana nazo. Leo hii kuna watu walioziba masikio na mioyo yao. Ni watu wasiokuwa tayari kumsikiliza na kufuata amri, sheria na maagizo ya Mungu katika maisha yao ni watu wanaotaka kuishi kana kwamba, hakuna Mungu na kama yuko atajitetea mwenyewe.

Matokeo yake ni ubinafsi, ukanimungu, kiburi na hali ya kutojali amri na maagizo ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Askofu Ngalalekumtwa anasikitika kusema hivi ni vikwazo kwa familia kuweza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika maisha na utume wake. Hapa, kuna haja ya kuendelea kukazia toba na wongofu wa ndani, ili kutambua na kushuhudia uwepo wa Mungu katika historia na maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.