2016-06-18 16:50:00

Shuhudieni umoja na mshikamano wa Kanisa kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa!


Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani ya Kanisa ambamo waamini wanaalikwa kumtukuza Mungu kwa kuonesha umoja na mshikamano wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa. Umoja huu unapata ushuhuda wake kwa kuungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, mwamba wa Kanisa la Kristo na changamoto ya kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia pamoja na kuendeleza mchakato wa Utamadunisho wa Injili katika tamaduni na mila za watu wa mataifa.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu huko Leopoli, nchini Ukraine, Jumamosi, tarehe 18 Juni 2016. Amesema, vita, nyanyaso na dhuluma zinazofanywa dhidi ya watu ni dalili za binadamu kushindwa kuheshimu utu na heshima ya binadamu na kwamba, haya ni matokeo ya uchu wa mali, madaraka na ubabe badala ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu wa binadamu na kushuhudia Injili ya uhai.

Hata katika mateso kama haya, binadamu anapaswa kukumbuka kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kumlinda na kumtetea na kwamba, Mungu ndiye anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu. Wananchi wa Ukraine wameshuhudia wenyewe jinsi ambavyo watu wamekengeuka na kumezwa na malimwengu kiasi cha kupandikiza utamaduni wa kifo; ukosefu wa uaminifu, uadilifu na mafao ya wengi na kwamba, si rahisi kuweza kumtumikia Mungu na mali. Inasikitisha kuona kwamba, katika ulimwengu mamboleo utajiri wa dunia unamilikiwa na watu wachache wakati kuna mamillioni ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, umaskini na magonjwa na matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kimamii.

Kardinali Parolin anawataka viongozi wa Kanisa kutambua kwamba, wamepewa dhamana na wajibu wa kulinda na kusimamia mali ya Kanisa; watambue kwamba, wao wanapaswa kujitofautisha na viongozi wa dunia, kwa kutumia vyema mali ya Kanisa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kuwashirikisha watu furaha inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Watu wanaoteseka kwa vita, dhuluma na nyanyaso watambue kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau, iko siku atawashangaza!

Waamini wanahamasishwa kutafuta, kuendeleza na kudumisha Ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote watapewa kwa ziada. Hii ni changamoto ya kuachana na vita, nyanyaso na dhuluma, ili kuambata wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kanisa litaendelea kuonesha mshikamano wa udugu na upendo kama kielelezo cha imanai tendaji. Fumbo la Pasaka ni ushuhuda wa mshikamano wa Kristo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hili ndilo chimbuko la Kanisa linalofumbatwa katika imani inayosimuliwa na kushuhudiwa katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.