2016-06-18 07:03:00

Papa asema: Familia, Ushuhuda na Unabii muhimu katika Uinjilishaji!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi usiku tarehe 16 Juni 2016 amezindua maadhimisho ya Kongamano la Jimbo kuu la Roma yanayoongozwa na kauli mbiu “ Furaha ya upendo: Hija ya familia za Roma mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: Utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; kishawishi cha kutaka kuwatenga wengine badala ya kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana pamoja na umuhimu wa wazee katika jamii, kwani wao wana ndoto za kinabii!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Kongamano hili la Kijimbo litawasaidia washiriki kuweza kufahamu mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Sinodi za Maaskofu kuhusu maisha na utume wa familia, kwa kuwa na ujasiri wa kusikiliza na kuzisaidia familia zinazoogelea katika dimbwi la shida na mahangaiko mbali mbali. Mababa wa Sinodi katika tafakari zao, mbele ya macho yao walikuwa na familia zilizokuwa zinahitaji kuheshimiwa kutokana na utakatifu wao.

Lengo kuu lilikuwa ni kusikiliza kile ambacho Mwenyezi Mungu atakakuwaambia waja wake katika mazingira kama haya, ili hatimaye, Kanisa kuweza kuibuka na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, sanjari na kutegemea neema ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, yote haya yanaweza kufanyika ikiwa kama waamini watajikita katika imani, ili kutambua uwepo wa Mungu katika mageuzi ya kihistoria.

Kila mtu katika maisha, ameweza kujipatia mang’amuzi ya kifamilia yanayojikita katika furaha na shukrani; shida na magumu ya maisha, lakini ikumbukwe kwamba, familia si tatizo bali ni fursa na changamoto inayolitaka Kanisa kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi, ili kuweza kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi kama inavyotakiwa kwa Jimbo kuu la Roma. Lengo ni kupyaisha matumaini na utambuzi kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda kazi ndani ya familia, changamoto na mwaliko wa kuwaambata wote bila kuwatenga wengine katika maisha na utume wa Kanisa, ili wote waguswe na ndoto ya Mungu. Jambo hili linawezekana katika imani na kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu, ili kutambua kwamba, Mungu yupo, anaishi na kutenda; ameteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu anasema, Pili, kuna kishawishi kikubwa kwa baadhi ya waamini kudhani kwamba, wao ni watakatifu na bora zaidi kama ilivyokuwa kwa yule Mfarisayo aliyejikweza alipokuwa anasali. Hapa watu wana amini kwamba, kwa njia hii wataweza kupata utambulisho na usalama, pale wanapokuwa tofauti na wengine. Hapa kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kuendelea kurudia tena na tena maagano na Mungu kwa kumwomba huruma na msamaha; hali inayofumbatwa katika unyenyekevu na utamaduni wa kusikiliza.

Jicho la huruma ya Mungu liwawezeshe waamini kuona ukweli wa maisha na utume wa familia kwa nyakati hizi; familia ambazo zinakabiliwa na dhambi pamoja na changamoto mbali mbali za maisha, lakini kila tukio ni fursa y akujenga madaraja ya kukutana na watu sanjari na kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Yesu analitaka Kanisa kuonesha ile sura ya Mama mpendelevu, anayejali na kuguswa na mahangaiko ya watoto wake. Baba Mtakatifu anasema hapa waamini waoneshe moyo wa huruma na mapendo, badala ya kuhukumu na kulaani wengine, wajenge ndani mwao huruma kama ile ambayo Yesu alionesha katika maisha na utume wake hapa duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tatu, Mababa wa Sinodi walikazia kwa namna ya pekee ushuhuda wa maisha unaotolewa na wazee wenye ndoto za kinabii wakati vijana wana mwono wa maisha. Ushuhuda ni mahali ambapo waamini wanaweza kugundua mpango wa Mungu katika maisha ya watu. Roma kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya vijana wengi kutokuwa na matumaini wala fursa za ajira; mambo yanayogumisha maamuzi ya vijana hawa katika maisha ya ndoa na familia. Lakini bado kuna waamini wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya ndoa, kielelezo cha uaminifu, udumifu na upendo usiochujuka.

Wazee ni vyombo na mashuhuda wa kinabii, changamoto kwa jamii kuwaheshimu na kuwathamini, badala ya kuwatenga na kuwatelekeza kama magari mabovu! Vijana wasipokuwa na mifano bora ya kuiga watakosa: imani, uhakika wa usalama katika maisha yao na hatimaye, kutumbukia katika woga na wasi wasi wa maisha. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa hekima na busara kutoka kwa wazee kama ilivyokuwa kwa Yesu alipopelekwa Hekaluni. Waamini walei wawe na ujasiri wa kurithisha imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuendeleza mema na matakatifu katika jamii. Huu ni muda wa wazee anakaza kusema Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya Wosia wa Kitume, “Furaha ya Upendo ndani ya familia” unahimiza pamoja na mambo mengine: umuhimu wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo: sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wale ambao wako pembezoni mwa jamii, ili waonje na kuguswa na huruma ya Mungu na mwishoni, wazee wapewe nafasi ya kushirikisha unabii wao katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuendeleza utume wa familia kwa kujikita katika: kupokea, kusindikiza, kung’amua na kushirikisha, mambo ambayo yamechambuliwa kwa kina na mapana katika wosia huu wa kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.