2016-06-18 08:39:00

Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma ya Mungu!


Majuma matatu yaliyopita tumesherehekea Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Masomo ya Dominika ya leo yanatuletea kwa namna fulani utajiri uliofichika katika Moyo huu Mtakatifu wa Mwokozi na tunapokuwa tayari kuelekeza macho yetu katika moyo huo tunakuwa na furaha na kama Mungu anavyotuambia kwa kinywa cha Nabii Isaya kwamba “kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu” (Is 12:3). Si lengo langu katika tafakari hii kurudia kuitafakari sherehe hiyo bali nimeona ndani ya tunu hiyo ya kimbingu tunaweza kuchota elimu ya kutosha inayotolewa na masomo ya Dominika hii, yaani juu ya ukweli kuhusu Yesu Kristo Mwokozi wetu ambaye anatufunulia huruma ya Mungu kwa njia ya mapendo yake yasiyo na kipimo. Dominika hii tunaalikwa kutafakari juu ya ukweli huo wa mapendo ya Mungu na kisha kutoka na elimu hiyo tukakayoichota na kuidhihirisha kwa wengine katika maisha yetu ya ufuasi.

Mnamo mwaka 1956 Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili aliandika waraka wake ulioitwa “Mtateka maji” “Haurietis Aquas”ikiwa ni kuadhimisha miaka mia moja tangu vuguvugu la heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu lilipoanza. Waraka huo unamwalikwa mwanadamu kujifunua katika fumbo la Mungu na mapendo yake na kukubali kuundwa upya kwa njia ya fumbo hilo. Ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, anasema Baba Mtakatifu, tunauonja upendo wa Mungu ambaye amemtoa mwanae wa pekee ili atukumboe sisi wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Ni katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ndipo tunaipata elimu iliyo sahihi kuhusu Mungu na uzito wa mapendo yake kwetu sisi wanadamu.

Katika Injili ya leo Kristo anawauliza Mitume wake swali la msingi sana, yaani ni kwa namna gani yeye anaeleweka kwa watu wengine na hata kwa mitume wenyewe. Uelewa wetu huo kuwa Kristo ni nani ni msingi thabiti kwa maisha yetu ya kikristo. Jibu la Petro kwamba “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu” linaweza lisieleweke kwa haraka sana na pia linaweza lisitufunulie kinagaubaga ni nini inapaswa kuwa mwitikio wetu kwa kukiri imani hiyo, mwitikio ambao unapaswa kuutilia muhuri wito wetu wa kikristo. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ametuambia kwamba “tunaweza kwa dhati kuwa Wakristo kwa kuelekeza macho yetu juu ya msalaba wa mkombozi, ‘kwake yeye waliyemtoboa”, tunapoelekeza macho yetu katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Yesu kama anavyokiri Petro ni Kristo wa Mungu, yaani ni mpakwa mafuta wa Mungu. Tendo hili la kukiri imani la Petro linamfanya Kristo kufafanua zaidi nini maana ya huko kupakwa mafuta kwake. Kristo huyo “atapata mateso mengi, atakataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, atauwawa na siku ya tatu atafufuka”. Tunapokwenda ndani zaidi na kujiuliza kwa nini aliuwawa tunaona ni kwa sababu ya chuki dhidi ya ukweli, chuki ambayo imeendelea kuwafanya wanadamu kuendelea kuwa watumwa wa dhambi. Ukinzani huu unapata mizizi yake katika dhambi ya asili: “Adamu ... uko wapi ... nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha” (Mw 3:9- 10).

Uwepo wa ukweli wa Mungu unamkimbiza mwanadamu na kuendelea kumfanya mtumwa wa dhambi. Lakini upendo wa Mungu unaendelea kuwaka dhidi ya mwanadamu, kwa njia ya neema yake anamfanya aangalie nyuma na kuona jinsi alivyopotea. Mwanadamu anavyogeuka nyuma na kumtazama yule waliyemchoma kama anavyoagua Nabii Ezekieli katika somo la kwanza anaingia katika hali ya maombolezo, anajiona alivyopotea na kama Wimbo wa Zaburi anaanza kulia akisema “Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, katika chi kame ya uchovu, isiyo na maji”.

Mwanadamu anapoendelea kuinua macho yake na kumwelekea huyu aliyetobolewa anapata fursa ya kutafakari Upendo mkubwa wa Mungu na zaidi anaingia ndani na kujifungamanisha na upendo huo. Hapa ndipo unapozaliwa wito wetu wa kikristo. Tunapochota elimu hiyo ya kimungu haiishii tu katika akili zetu na kupanua uelewa wetu bali inatupeleka katika kutumwa na kutenda mithili ya Kristo aliye “ufunuo wa uso wa huruma wa Baba”. Hivyo ufuasi wetu unajengeka katika hali hiyo ya kujimithilisha na Kristo na kuwa tayari kuangamiza nafsi yetu kwa ajili yake.

Changamoto nyingi za maisha ya mwanadamu leo hii zinapata suluhisho lake hapa. Ni kwa njia hii ya mwanadamu kukubali kuinua uso wake na kumwangalia Yeye alitobolewa ndipo atakapoelewa ukweli juu ya upendo wa Mungu dhidi ya upotofu wa mwanadamu. Fundisho analotupatia huyu Kristo wa Mungu ambaye ndiye anayetobolewa ni upendo na kutekeleza yote kadiri ya ukweli ambao ni upendo wa Mungu. Kila kadhia katika maisha yetu inaashiria kupindishwa kwa ukweli huu na kama nilivyoeleza hapo juu dhambi ya asili inaendelea kumwandama mwanadamu na kumkimbia mwenyezi Mungu, kitendo ambacho daima hakimpatii suluisho la kudumu.

Neno hilo la kuwa tayari kuangamiza nafsi linatudai kuwa tayari kuuvua utu wetu wa kidunia na kujivika utu mpya katika Kristo. Utu huo wa kidunia ni ule ambao daima unatufanya kuendelea kuwa na kiu katika mambo ya ulimwengu huu: mali, vyeo, madaraka na pesa. Tunaendelea tu kuelekea kisimani mithili ya yule mama Msamaria tumsikiaye katika somo la Injili ya Mtakatifu Yohane Lakini tunapokutana na Yesu yeye anatupatia maji ambayo yanatufanya tusiwe na kiu tena. Hivyo mmoja anakuwa tayari kupoteza jina lake, nafasi na mamlaka yake, mali zake na hata kutoa mali zake zote kwa ajili ya Kristo na Kristo anatuambia kwamba huyu ndiye atakayeisalimisha nafsi yake.

Dominika ya leo inatualika kuingia katika fumbo la Kristo na kuelewa kwa mapana na urefu wake utajiri wa Upendo wa Mungu uliofichika ndani mwake. Baada ya hatua hii tuandae udongo mzuri wa kuudhihirisha upendo huo katika maisha yetu kwa kuwa vyombo vya kuieneza huruma ya Mungu kwa wengine. Moyo wa Yesu wenye uvumilivu na huruma nyingi, tajiri kwa wote wenye kukuomba na chemchemi ya uzima na utakatifu, utuhurumie.

Kutoka Studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha, Tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus!








All the contents on this site are copyrighted ©.