2016-06-18 09:04:00

Jumuiya ya Domenico Tardini na huduma kwa vijana


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 18 Juni 2016 anatarajiwa kutembelea Makazi ya Nazaret ambako atakutana na kuzungumza na wanafunzi, wanajumuiya na viongozi wa Jumuiya hii na baadaye, atafafanya nao tafakari juu ya Msamaria mwema na hatimaye kujibu baadhi ya maswali yatakayoulizwa na wanajumuiya hao.

Itakumbukwa kwamba, Makazi haya yaliundwa kunako mwaka 1946 na Monsinyo Domenico Tardini ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Kardinali kwa ajili ya kupokea na kutoa hifadhi kwa watoto yatima, familia zenye watoto wengi na maskini, ili kutambua na kuenzi wito na dhamana yao katika maisha, utume na mafao ya jamii nzima. Kunako tarehe 13 Januari 1963 Papa Yohane XXIII akaunda Mfuko wa Familia Takatifu ya Nazareti, unaojulikana kama “Villa Nazareth”.

Tangu mwaka 1969 makazi haya yakawa ni chemchemi ya umoja, upendo, udugu na mshikamano kati ya vijana wa kizazi kipya wanaoogelea katika dimbwi la shuda na mahangaiko yao ya ndani, wafanyakazi pamoja na marafiki wa Kardinali Tardini, wote hawa wanapenda kushirkishana Injili ya furaha, imani na matumaini, hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Kutokana na mshikamano huu, kunako mwaka 1980 kukaanzishwa Jumuiya ya Domenico Tardini inayotoa nafasi ya malazi kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na kuwapatia fursa ya kupata majoundo makini katika maisha ya Kikristo. Huu ndio ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, hususan wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Tarehe 24 Mei 2004, Baraza la Kipapa la Walei likakiitambua “Jumuiya ya Domenico Tardini” na kuipatia hadhi ya kimataifa na haki za kipapa. Jumuiya hii inajikita katika huduma ya kiuchumi na maisha ya kiroho kwa kuwapatia vijana nafasi ya masomo na kwamba, inatambuliwa pia na Serikali ya Italia. Vijana hawa wanapata nafasi ya kuweza kushirikisha karama, ujuzi na maarifa pamoja na vijana wenzao, huku wakiwajibika barabara katika maisha ya kijamii sanjari na kuendelea kufundwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo!.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.