2016-06-16 07:26:00

Yesu Kristo ni ufunuo wa huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha toba na wongofu wa ndani; ni wakati wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo; kwa kujenga na kuimarisha mahusiano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na utume huu kadiri ya maisha, wito na nafasi yake ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Lengo ni kuwasaidia waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, furaha, amani, udugu, wema na uzuri kwa watu wanaowazunguka.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wasaniii wa mitaani. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Trastevere, lililoko mjini Roma.

Katika maadhimisho haya, wasanii na wanamichezo hawa, wameishirikisha familia ya Mungu Roma, ile furaha ya imani inayofumbatwa katika michezo ya kuigiza, sarakasi na sanaa, kielelezo makini cha taaluma na weledi katika shughuli zao zinazowapatia riziki yao ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko ni mfano na kielelezo cha Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Anathamini na kuheshimu mchango unaotolewa na wasanii katika maisha ya kijamii, mwaliko kwa wasanii pia kumshindikiza Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na maombi yao.

Kardinali Vegliò anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa muafaka ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa njia ya Yesu Kristo, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, aliyekuja duniani ili kuwakomboa watu wake, kwa neno lake, matendo yake na kwa nafsi yake na kwa njia hii ameifunua huruma ya Mungu kwa binadamu wote. Amewatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, wafungwa kufunguliwa kwao na wale waliosetwa kuachiwa huru pamoja na kuutangaza Mwaka wa Bwana.

Kwa njia hii, Yesu alifunua utambulisho wake, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujitambulisha na Yesu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini waguswe na Neno la Mungu, wawe tayari kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kuonesha huruma na mapendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na upatanisho na Mungu pamoja na jirani zao, dhamana inayohitaji kwa namna ya pekee uwazi pamoja na kukimbilia kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na faraja ya Mungu kwa watu wake.

Wasanii hawa wamekumbushwa kwamba, maisha na utume wao unawasukuma kuwa ni mashuhuda na manabii wa matumaini, kwa kuwawezesha watu wengine kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu kwa njia ya jirani zao. Kwa kazi zao, wawaonjeshe watu furaha, waelimishe umuhimu wa umoja na mshikamano wa kidugu; wawathamini wanyonge na wahitaji katika maisha kwa kutambua kwamba, wote wanahitajiana na kukamilishana katika hija ya maisha yao ya kila siku. Wamwambate Mungu ili waweze kushiriki kikamilifu katika kazi yake ya ukombozi.

Kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, walau anatekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia pia ya kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Dhamana hii inahitaji ujasiri, moyo wa huruma na mapendo, sadaka na majitoleo yanayojikita katika imani tendaji, bila ya kukata tamaa hata kama kuna vikwazo na magumu ya maisha. Yote haya, Kardinali Antonio Maria Vegliò anayaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya na Mama wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.