2016-06-16 08:07:00

Mshikamano wa upendo na udugu kwa wananchi wa Equador na Colombia


Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameguswa na mateso na mahangaiko ya Familia ya Mungu nchini Equador na Colombia, walioguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao, ametuma ujumbe wa mshikamano na upendo wa kidugu kwa wananchi wa maeneo haya, ili kuonesha uwepo wake wa karibu katika shida na mahangaiko yao.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu nchini Equador na Colombia kuanzia tarehe 16- 24 Juni 2016 na utakuwa chini ya Monsinyo Segundo Tejado Munos, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Zaidi ya watu mia sita walifariki dunia na wengine wengi hawana makazi maalum.

Tayari Cor Unum ilikwisha kupeleka msaada wa dharura, lakini kwa sasa wanataka kufanya upembuzi yakinifu ili kuangalia ni mahali gani Vatican inaweza kusaidia mchakato wa huduma kwa waathirika, hususan katika ujenzi wa shule, makazi ya watu na majengo ya huduma. Taarifa kutoka Equador zinaonesha kwamba, bado kuna watu wengi ambao hawana tena nishati ya umeme, maji safi na salama, huduma za afya na elimu na kwamba, bado watu wengi wanakabiliwa na wasi wasi wa magonjwa ya mlipuko.

Kuanzia tarehe 21- 24 Juni 2016 ujumbe wa Cor Unum utakuwa nchini Colombia, ili kushiriki katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu Amerika ya Kusini, ulioanzishwa kunako mwaka 1992 na Mtakatifu Yohane Paulo II na kuukabidhi chini ya usimamizi wa Cor Unum. Wajumbe wa mkutano huu watapembua na hatimaye kuidhimisha miradi itakayofadhiliwa na mfuko huu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi huko Amerika ya Kusini na Caraibi kwa Mwaka 2016. Hadi sasa kuna miradi 90 iliyokwisha wasilishwa inayogharimu kiasi cha dolla za kimarekani millioni moja na nusu. Itakumbukwa kwamba, wafadhili wakuu wa Mfuko huu ni Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.