2016-06-15 14:48:00

ROACO: Vipaumbele: huduma kwa wakimbizi na majiundo makini!


Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inapaswa kushughulikiwa kijami, lakini pia Kanisa linawajibika kiroho na kimaadili kuwahudumiwa watu hawa kwa kuthamini mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa, hususani, amana yao katika masuala ya kiliturujia, kitaalimungu na kinidhamu. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki , Jumanne, tarehe 14 Juni 2016 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 89 wa Shirika la Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO.

Kardinali Sandri amekazia umuhimu wa Kanisa kuendeleza mchakato wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, ili kukomaza umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa ambalo kimsingi ni mchumba wa Kristo. Mchakato huu hauna budi kufumbatwa katika majiundo makini ya awali na endelevu ili kuliwezesha Kanisa kuwa na viongozi walioandaliwa barabara kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa sanjari na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kuendelea kujisikia nyumbani, hata wanapokuwa ugenini.

Kardinali Sandri anasema, majiundo makini na awali ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali, ili kuwawezesha majandokasisi na wakleri kutoka katika Makanisa ya Mashariki wanaosoma na kuishi ndani na nje ya Roma. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki linaendelea kuunda mazingira yatakayosaidia Wakleri kutoka Mashariki kupata huduma makini wanapokuwa masomoni hapa Roma. Haya ni majiundo yanayojikita katika huduma ya upendo. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na majiundo makini kwa walezi na uchaguzi makini kwa watu wanaoomba kuwekwa wakfu kama Mapadre na Watawa.

Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki litaendelea kushirikiana pia na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri na Waseminari, ili kuhakikisha kwamba, walengwa wanapatiwa malezi na majiundo makini katika maisha na utume wao, ili Kanisa liendelee kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika huduma makini. Mkutano huu ni wa mwisho, kabla ya kuanza maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia moja tangu kuundwa kwake na Papa Benedikto XV kunako tarehe 1 Mei 1917, baada ya kuchapisha barua yake binafsi ijulikanayo kama “Dei providentis”. Maandalizi ya maadhimisho haya yanaanza kufanyiwa kazi kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.