2016-06-15 10:10:00

Kipofu wa Yeriko shuhuda wa mwanga wa huruma ya Mungu!


Huruma ya Mungu ni mwanga katika maisha ya mwanadamu kama ilivyojionesha kwa yule kipofu wa Yeriko aliyekuwa anaketi njiani kuomba sadaka kwa wapita njia, ili kujipatia riziki yake, kielelezo cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili; watu wanaotengwa na jirani zao, ingawa wako barabarani lakini hawana fursa ya kujenga daraja la kukutana na watu wengine, hapa barabara inakuwa ni kielelezo cha upweke hasi, unaoujaza moyo machungu ya maisha.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 15 Juni 2016 kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi ya kina wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anasema, mji wa Yeriko ulikuwa ni Lango la kuingilia katika nchi ya ahadi, mahali ambapo Musa aliwataka Waisraeli kutokuwa na shingo wala mioyo migumu kwa ndugu zao maskini, kwani hawa ni watu ambao kamwe hawatakosekana kwenye uso wa nchi, kama kielelezo makini cha kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani.

Kipofu wa Yeriko aliposikia kwamba, Yesu anapita katika njia ile akapiga kelele, “Yesu Mwana wa Daudi, Unirehemu”! Watu walitaka kumnyamazisha kwani alikuwa anasumbua, lakini akapaaza sauti yake zaidi. Hawa ni watu ambao wamekuwa ni vikwazo kwa ndugu zao kiasi cha kuwakataza wengine kumwona na kumfahamu Yesu. Lakini hata katika umati huu mkubwa ambao haukuwa umeguswa na mahangaiko ya Kipofu wa Yeriko, kulikwepo Msamaria mwema, aliyemwelezea yule Kipofu yale yaliyokuwa yanajiri kwa wakati huo, kama ilivyokuwa kwa Malaika wa Bwana wakati wa Pasaka alipowaokoa Waisraeli.

Kipofu wa Yeriko, hakufungwa mdogo na makundi ya watu, akaendelea kupiga ukelele, akiomba huruma kwa Yesu ili apate kuona tena, tayari alikuwa na jicho la imani na alitamani kumwona Yesu ambaye alimhurumia, akamshika mkono na kumweka kati kati ya umati ule mkubwa ili kumtangazia Habari Njema na kumpatia kipaumbele cha pekee, kipofu ambaye alikuwa ametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Kipofu akaweza kufunguliwa macho na kuanza kuelekea katika njia ya Wokovu, kwani hapo anakutana na huruma ya Mungu inayofariji na kuokoa.

Yesu mbele ya yule Kipofu wa Yeriko alionesha unyenyekevu mkubwa ili kumhudumia mgonjwa na mdhambi anayemtambua Kristo kuwa ni Bwana anayemkirimia tena uwezo wa kuona na kumshangilia Mungu; anajisikia kupendwa upeo na Kristo Yesu, kiasi cha kuamua kubwaga manyanga na kumfuasa Kristo kama shuhuda na mtume wake, tayari kujiunga na Jumuiya ya waamini wa Yesu. Huyu ndiye shuhuda aliyewasaidia watu wengine kupata mwanga wa kumwona Yesu kwa jicho la imani na hivyo kujiunga naye katika sala na masifu. Baba Mtakatifu anasema, hivi ndivyo Yesu alivyoeneza huruma na upendo wake kwa wale wote waliobahatika kukutana naye; akawaita na kuwakusanya; akawaponya na kuwaangazia, kiasi cha kuunda watu wapya wanaoadhimisha matendo makuu ya upendo wa huruma ya Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya jirani zao.

Mwaka wa huruma ya Mungu kiwe ni kipindi cha neema na upyaisho wa maisha ya kiroho. Iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha imani na upendo wa kidugu, tayari kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu inayoleta mabadiliko katika maisha ya watu kwa kusamehe na kuangalia wema zaidi. Watu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.