2016-06-14 09:04:00

Tushikamane kuwafunda watanzania katika uadilifu ili wasitumbuliwe!


Mtumishi wa Mungu huitwa sio sababu ya haiba, taaluma, ubora alio nao bali kwa upendo wa Mungu. Na ingawa huwa mnyonge na dhaifu, Mwenyezi Mungu humuwezesha kwa matunda anayomkirimia ndani yake kama alivyomthibitishia Nabii Yeremia: “Tazama nimetia Neno langu ndani yako”. Msingi wa kuitwa na kutumwa huko ni Sakramenti ya Ubatizo ambapo kila mbatizwa huitwa kuwa shahidi wa kiini cha Imani, Fumbo la Pasaka: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ameyasema hayo Askofu Mkuu wa Mwanza Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, katika maadhimisho ya kumuweka wakfu na kumsimika Askofu Flavian Matindi Kassala jimboni Geita, Tanzania, Jumapili 12 Juni 2016.

Waamini wa Jimbo la Geita wamekuwa na changamoto na hamu ya kuwa na mchungaji mkuu tena, baada ya aliyekuwa Askofu wa jimbo hilo kuhamishiwa Jimbo kuu la Songea, Mhashamu Damian Dallu. Mahangaiko pengine na kukata tamaa kama wanafunzi wa Yesu walipoamua kwenda kuvua samaki tena pale ziwa la Tiberia. Maamuzi ya kurudia mazoea ya kale. Kristu anawaalika kwa upendo kuyachangamkia matunda ya ufufuko na sio kukata tamaa. Anamuweka Askofu Kassala kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo hilo na kuwaalika washirikiane naye bila woga wala makundi ndani ya Jimbo.

Askofu Kassala anapoitwa kuwa mrithi wa kazi ya kitume, anaalikwa kulilisha Neno kundi la Mungu Geita. Atafanya hivyo kwa uaminifu na uthabiti kadiri ya mapenzi ya Mungu na sio porojo na udaku kama wafanyavyo manabii wa uongo. Atalichunga kundi hilo akiliepusha na hatari, akifuata nyayo za mchungaji mwema, Yesu Kristo wenyewe anayemshirikisha uchungaji huo. Tatu atalitakatifuza kundi hilo akiuchukua Msalaba wa Kristo vizuri bila kuuburuza. Askofu Mkuu Ruwa’ichi amemhakikishia Askofu Kassala: urafiki, upendo na ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu Mkuu Francesco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania anayemaliza muda wake amemtaka Askofu Kasala kuitazama dunia yenye changamoto nyingi na inayohangaika kupata jibu ambalo ni huduma ya upendo na huruma hasa kwa vijana.

Akitoa Shukrani zake, Askofu mpya Flavian Kassala ameialika familia ya Mungu Jimboni Geita kuungana naye katika huduma ya upendo na umoja wakiutazama Uso wa Huruma ya Mungu katika awamu hii ya tatu ambapo Jimbo la Geita linapata Askofu mwingine. Analialika Kanisa zima la Tanzania kuungana ili kuendeleza mchakato wa ukombozi: kiroho na kimwili, ili watanzania waweze kuwa ni raia wema, waadilifu na wenye upendo kati yao na wala si majipu ya kutumbuliwa! Wawe kweli ni raia wenye uzalendo na uchungu kwa nchi yao.

Jimbo la Geita lilitangazwa rasmi mwaka 1985 na Askofu wake wa kwanza akiwa Aloysius Balina. Baada ya miaka kumi na miwili, alihamishiwa Shinyanga na akasimikwa Askofu Damian Dallu. Mnamo 1914 Askofu Dallu alihamishiwa Jimbo kuu la Songea, na sasa Jimbo la Geita limempata Askofu Flavian Matindi Kassala. Itakumbukwa kwamba, Ibada ya kumweka wakfu na hatimaye kumsimika Askofu Kassala ilitanguliwa na Masifu ya jioni yaliyoongozwa na Askofu mkuu Damian Dallu wa Jimbo kuu la Songea.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.