2016-06-14 06:36:00

Askofu mkuu Peter Wells ateuliwa kuwa Balozi wa Vatican Swaziland


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Peter Bryan Wells kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Swaziland. Ataendelea pia kuwa ni Balozi wa Vatican Afrika ya Kusini, Bostwana, Lesotho na Namibia. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Wells alizaliwa tarehe 12 Mei 1963 huko Oklahoma, Jimbo Katoliki la Tulsa, Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 12 Julai 1991 akapewa Daraja takatifu la Upadre.

Askofu mkuu Peter Bryan Wells alianza utume wake katika kada ya kidiplomasia mjini Vatican kunako tarehe 1 Julai 1999 na mara moja akatumwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Nigeria. Baadaye akarejeshwa mjini Vatican kama afisa mwandamizi wa Sekretarieti ya Vatican. Kunako tarehe 9 Februari 2016, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican Afrika ya Kusini na Bostwana na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko akamweka wakfu kuwa Askofu mkuu hapo tarehe 19 Machi 2016, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mchumba wa Bikira Maria na msimamizi wa Kanisa sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Papa Francisko alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro hapa mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.