2016-06-13 15:13:00

Papa awapongeza wafanyakazi wa WFP katika mapambano dhidi ya njaa


Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wafanyakazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Jumatatu tarehe 13 Juni 2016 aliomba radhi kwamba, alikuwa amepanga kuwahutubia kwa lugha ya Kihispania, lakini kutokana na wengi wao kufahamu zaidi lugha ya Kiitalia, basi akaamua kuwapatia hotuba yake iliyoandikwa na baadaye kuwashirikisha mambo makuu yaliyokuwa yamefichama katika sakafu ya moyo wake. Amewakumbusha kwamba, wao kama wafanyakazi ni nguzo thabiti inayosimamisha mipango na utekelezaji wa sera na mikakati mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani. Huu ni wajibu ambao wafanyakazi hawa wanautekeleza kwa ari, sadaka na moyo mkuu sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wazazi na walezi wao, wanaowawezesha kutekeleza vyema zaidi huduma kwa watu wanaoteseka na baa la njaa duniani, hata kama hawamo kwenye orodha ya wafanyakazi wa  Shirika la Mpango wa Chakula Duniani. Hii ni kazi ndogo inayojikita katika sadaka, kiasi cha kuwawezesha watoto wengi walau kupata chakula cha msaada, tayari kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani.

Baba Mtakatifu anawapongeza wafanyakazi hawa kutokana na ushujaa na ushupavu wao wa kuendelea kuhudumia pasi na kukata tamaa, wote kwa pamoja wakiunda na timu moja ya kazi, inayowashirikisha wote. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea mashuhuda wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani. Hawa ndio wale ambao majina yao yameandikwa kwenye lango la kuingilia kwenye Makao makuu ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani. Mashuhuda hawa wameweza kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuwa walikuwa ni watu imani, waliotambua na kuthamini umuhimu wa kazi iliyokuwa inasindikizwa na wafanyakazi wengine. Baba Mtakatifu aliwashukuru na kuwaomba wazidi kumwombea katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.