2016-06-13 15:27:00

Jengeni madaraja ya huduma yanayofumbata uso wa mwanadamu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 13 Juni 2016 mara baada ya kuzungumza na viongozi wakuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika hili pamoja na familia zao kwa kuwashukuru kwa huduma makini ya upendo na mshikamano wanayoitoa kwa waathirika wa baa la njaa la umaskini duniani; wao ni vielelezo vya nyuso za mshikamano; dhamana wanayoitekeleza kwa weledi, sadaka, ukarimu na hata wakati mwingine wanajikuta wakiwa kwenye mazingira magumu na hatarishi.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi hawa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila hata ya kujibakiza, daima wakiwa tayari kuhudumia. Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kuwa na majiundo endelevu yanayojikita katika huruma ili kutoa maana kamili ya kazi kubwa wanayoendelea kuitekeleza, dhamana nyeti katika maisha ya mwanadamu. Wafanyakazi wa WFP wajitahidi kushinda kishawishi cha uvivu na uzembe kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi, weledi, sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani.

Wamekumbushwa kwamba, hawa ndio wanaowahamasisha kuwapatia kipaumbele cha pekee kwa kutambua kwamba, kila ukurasa una historia nyeti na inayofumbatwa na machungu katika maisha, hali inayoonesha sura na mateso ya watu wanaoomba msaada wa chakula. Wafanyakazi hawa wakijenga utamaduni wa kusikiliza kilio cha maskini, wataweza kuwa na ujasiri wa kuvunjilia mbali sera na mikakati baridi isiyokidhi mahitaji ya maskini, lengo ni kuhakikisha kwamba, baa la njaa linapewa kisogo!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, baa la njaa ni kati ya mambo ambayo yanahatarisha amani na utulivu kati ya watu; dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na kupatiwa jibu makini; kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana, wajibu na nafasi yake kikamilifu; hapa kila mtu anahusika na hakuna mtu awaye yote anayeweza kujiweka pembeni kwamba, hausiki na mapambano haya! Maendeleo makini ya kiutu, kijamii na kiuchumi ni muhimu sana katika harakati ya mtu, familia na jamii kuhakikisha kwamba, inajipatia mahitaji yake msingi, mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha, utu na heshima ya kila binadamu.

Hii ina maana ya kutoa chakula cha msaada kwa waathirika wa baa la njaa; kutoa msaada wa vifaa na ufundi; kutengeneza fursa za ajira; kutoa mikopo nafuu, ili kuwajengea watu mahalia uwezo wa kiuchumi wanapokabiliwa na majanga asilia. Dhamana hii inajikita pia katika wajibu wa kimaadili, ili kujenga na kudumisha mafao ya wengi kwa kila nchi na katika Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla wake.

Baba Mtakatifu anatambua shida na changamoto zinazoweza kuwaandama, lakini wasikate tamaa wala kuvunjika moyo; wawe na ujasiri wa kusaidiana na kuaminiana, ili kuondokana na kishawishi cha kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Anawataka kuendelea kujenga ulimwengu wenye uso wa binadamu unaofumbatwa katika: huruma na mshikamano; msaada na sadaka; ili kukuza ukarimu, ujasiri, imani pamoja na ushirikiano mpana zaidi ili kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu, tayari kujikita katika njia ya matumaini; usawa wa maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na kusimama kidete kupambana na ukosefu wa usawa kiuchumi, hali inayosababisha mateso makubwa kwa maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.