2016-06-12 10:37:00

Jengeni urafiki na udugu ili kuimarisha haki na amani jamii!


Kardinali Edoardo Menichelli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ancona-Osimo, Jumamosi jioni, tarehe 11 Juni 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya hija ya 38 ifanywayo na waamini kwa miguu kutoka Macerata hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa Mwaka 2016 ni “Wewe ni wa pekee kabisa”, maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyatoa hivi karibuni kwa mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kuwaonesha Uso wa huruma ya Mungu kwa kila mmoja wao. Mwanadamu anakumbushwa kwamba, anapendwa na ana thamani kubwa mbele ya Mungu, hazina ambayo kamwe haipaswa kufutika kama ndoto ya mchana!

Baba Mtakatifu kwa kutambua umuhimu wa hija hii kwa waamini wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha, amewapigia simu washiriki wa hija hii kwa kuwataka kupokea neema ya Mungu katika maisha yao na kutembea katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, imani ni hija inayomwilishwa katika maisha ya mwanadamu mintarafu ujenzi wa urafiki na udugu katika maisha ya kijamii, ili kweli kuimarisha jamii inayojikita katika haki na amani, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na kuwatakia furaha na matumaini, tayari kukutana na kumwabudu Yesu wa Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo wake endelevu kati ya waja wake. Baba Mtakatifu amehitimisha salam zake kwa njia ya simu kwa kuwatakia mahujaji wote hija ya maisha bila kusimama na hatimaye, kukata wala kujikatia tamaa, kwani huu ndio ukweli wa maisha. Anawaomba kumkumbuka katika sala na sadaka yao, ili asonge mbele katika maisha na utume wake kadiri ya utashi wa Kristo kwa Kanisa lake. Baba Mtakatifu amewatakia matembezi yanayojikita katika sala na furaha ya maisha; katika umoja na udugu, kwa kumwangalia Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa na katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kumpokea Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.