2016-06-11 10:52:00

Simameni kidete kudumisha Injili ya uhai, utu na heshima ya wagonjwa!


Madaktari na wauguzi ni watu wenye taaluma na wito wa kukuza na kudumisha Injili ya uhai na kamwe haiwezi kukubalika kwamba, taaluma hii itumike kwa ajili ya kupandikiza utamaduni wa kifo sanjari na kudhalilisha maisha, utu na heshima ya wagonjwa. Wafanyakazi katika sekta ya afya hawana budi kuwa makini ili kuhakikisha kwamba, taaluma yao kamwe haitumiki kwa ajili ya kuwanyanyasa wagonjwa kwa kuwatumbukiza katika dimbwi la kifo laini eti kama kielelezo cha huruma na faraja kwa wagonjwa wanaoteseka!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na Madaktari pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya kutoka Hispania na Amerika ya Kusini, walipomtembelea mjini Vatican. Huruma na upendo wa kweli, kamwe hauwezi kumtenga, kumdhalilisha wala kufurahia kifo cha mgonjwa, ambaye anapaswa kuwa ni kiini cha mchakato wa tiba. Huruma na upendo ni fadhila ambazo wagonjwa wanapaswa kuonjeshwa katika mahitaji yao kiroho na kimwili au kwa maneno mengine, wagonjwa wanapaswa kutendewa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, changamoto makini na endelevu inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, utamaduni mamboleo unaojengeka katika utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unagubikwa na ubinafsi na kwamba, fadhila ya huruma inaangaliwa kwa jicho la kengeza; maisha, utu na heshima ya mgonjwa si mali kitu! Hiki ndicho kielelezo cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Mafanikio ya mtu yanapimwa kutokana na mchango wake katika mchakato wa uzalishaji na utoaji huduma; afyua njema, utanashaji na uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii.

Baba Mtakatifu anawataka Madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja, huruma na mapendo kwa wagonjwa na wale wote wanapkimbilia msaada wao wa kitaaluma. Dhamana hii waitekelezwa kwa kujali kwanza kabisa utu, heshima na maisha ya wagonjwa; mambo msingi katika maisha ya mgonjwa. Madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya wajifunze utamaduni wa kuhudumia kwa ari na moyo mkuu, kielelezo cha huruma na mapendo kwa wagonjwa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anaona fahari na anapenda kubariki mikono ya madaktari wanaotoa huduma kwa ajili ya kudumisha Injili ya uhai ndani ya jamii, kielelezo cha huruma na upendo kwa jirani. Madaktari wanatakiwa kuachana na kishawishi cha kutekeleza dhamana na wajibu wao kama watu wa mshahara tu; watu wenye majibu ya mkato; wanaotafuta mali na madaraka ya chapuchapu. Huu ni mwelekeo potofu kwani hapa wanaweza kuchezea utu na heshima ya binadamu; dhamana na wito wa madaktari katika kuhudumia Injili ya uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.