2016-06-11 08:23:00

Siku ya wachangia damu duniani kwa mwaka 2016


Awali ya yote, napenda kuwashukuru kwa kujumuika nasi ili niweze kuongea na wananchi kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani. Kila mwaka tarehe 14 Juni, dunia inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa kuhusu huduma ya damu salama, kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari na pamoja na kuwatambua na kuwaenzi watu ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu. Aidha,Siku ya Wachangia Damu Duniani ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa ya Ndugu Karl Landsteiner, ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi ya damu ya “A”,”B” na “O”,na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo.

Ndugu Wananchi,

Mwaka huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama inatarajia kuadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani kwa kuhusisha Mikoa yote ambayo pia itashiriki katika kampeni ya Siku ya Wachangia Damu Duniani kwa kukusanya damu kila Mkoa, angalau Chupa za damu 100 kwa kila Halmashauri, Lengo ni kukusanya chupa 20,000 nchi nzima.

Kitaifa Maadhimisho haya yatafanyika tarehe 14/6/2016 hapa Mkoani Dodoma kwa kuhusisha vyuo vikuu vilivyopo Mkoani Dodoma, ambapo vitashiriki katika zoezi la kuchangia damu. Aidha, kilele cha maadhimisho hayo kitatanguliwa na kampeni ya siku mbili ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari na ukusanyaji wa damu. Ili kuendana na kauli mbiu ya ‘’HAPA KAZI TU’’ hakutakuwa na sherehe au shamrashamra zozote zaidi ya kukusanya damu.

Ndugu Wananchi,

Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “SOTE TUNAUNGANISHWA NA DAMU (BLOOD CONNECTS US ALL)”. Kauli Mbiu hiyo inalenga;

- Kuonyesha jinsi gani maisha ya watu yameweza kuokolewa na watu ambao wamekuwa wakichangia damu.

- Kuhamasisha wachangiaji damu wa kila mara, waendelee kuchangia damu.

- Kuhamasisha watu wenye afya njema ambao hawajawahi kuchangia wachangie damu.

- Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutambua wachangia damu wa kujirudia mara kwa mara na kuhakikisha upatikanaji wa damu na mazao ya damu ya kutosha kwenye hospitali zetu.

Ndugu Wananchi,

Maisha ya watu wengi yanaokolewa kila siku nchini kwa kuongezewa damu. Tunajua kwamba nchini Tanzania, kina mama wengi na watoto hupoteza maisha kwa kukosa damu salama. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, takribani wanawake 432kati ya vizazi hai 100,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi hapa nchini. Aidha, asilimia 80 ya hivyo vifo husababishwa na ukosefu wa damu salama wakati inapohitajika. Hali kadhalika ajali za barabarani haswa zitokanazo na bodaboda husababisha vifo na ongezeko la mahitaji ya damu, kwa mfano takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha ajali za barabarani zimesababisha vifo vya watu 3,468, na kati ya hivyo, vifo vya watu 934 (asilimia 27) vilisababishwa na bodaboda, na watu wengine 938 kujeruhiwa.

Ndugu Wananchi,

Ili kuhakikisha kuwa damu ya kutosha inakusanywa na kupunguza vifo vinatokanavyo na upungufu wa damu, Mpango wa Taifa wa Damu Salama unafanya kazi ya kukusanya damu kwa kushirikisha Halmashauri zote nchini. Huu ni mkakati ambao ulibuniwa ili kuongeza makusanyo ya damu ambayo mahitaji yake kwa mwaka ni chupa 450,000. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani mahitaji ya damu salama ni asilimia moja (1%) ya idadi ya watu wote. Mkakati wetu mpya wa kuhakikisha damu inakusanywa kwa kushirikisha Halmashauri pia umesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mkakati huu umeanza kuzaa matunda kwani taarifa ya robo mwaka (Januari - Machi 2016) inaonyesha jumla ya chupa za damu 42,978 zilikusanywa toka mikoa yote hapa nchini, ambayo ni asilimia 101 ya lengo la kukusanya chupa 42,500  Aidha, kwa mwaka 2016/2017 Mpango wa Taifa wa Damu Salama umejiwekea lengo la kukusanya chupa 300,000, ambapo kati ya hizo, chupa 160,000 zitakusanywa kwenye Kanda 6 za Mpango wa damu salama ambapo inakadiriwa chupa zipatazo 140,00 zitakusanywa na Halmashauri zote nchini.

Ndugu Wanahabari,

Wizara inatambua mchango wa wanahabari katika kuihabarisha jamii kuhusu huduma ya damu. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii yetu kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari. Moja ya changamoto za ukusanyaji wa damu salama ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu uchangiaji damu kwa hiari. Hivyo, tunaomba muendelee kutoa elimu na kuihamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji kuongezewa damu. Ninapenda kuwashukuru na kutambua wanahabari na vyombo vya habari ambayo vimekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kuhusu kucnagia damu kwa hiari. Tunawashukuru sana.

Aidha, Wizara yangu inatoa shukurani kwa wachangia damu mmoja mmoja na Taasisi mbalimbali zikiwemo shule, vyuo na madhehebu ya dini kwa ushiriki wao katika kuchangia damu. Pia, Natoa shukurani za dhati kwa mashirika mbalimbali kama Shirika la Marekani la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Dunia  (Global Fund) kwa misaada ambayo wamekuwa wakitoa kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika kuhakikisha upatikanaji wa damu salama nchini.

Aidha tunamshukuru Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa chupa zinazotumika kwa ajili ya kukusanya damu kwenye hospitali (blood collection tubes). Hakika uamuzi wake huu utaokoa maisha ya maelfu ya watanzania hasa wanawake wajawazito wanaofariki kwa kukosa damu. Tunamshukuru sana.

Hitimisho:

Damu salama ni muhimu katika utoaji huduma za Afya. Bila damu hakuna maisha, hivyo ni lazima tuhakikishe uwepo wa damu salama wakati wote kwenye Hospitali/Vituo vya kutolea huduma za Afya.  Kwa upande wetu Wizara ya Afya tutaendelea: Kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri wanaohusika katika ukusanyaji damu. Kuandaa miongozo mbalimbali inayotumika katika ukusanyaji damu ili kuboresha shughuli za ukusanyaji damu hasa kuhakikisha damu inayokusanywa na kuongezewa wagonjwa inakuwa salama katika nyakati zote. Kupima sampuli zote za Halmashauri kwenye maabara za Kanda. Na kufanya usimamizi shirikishi (Supportive supervision) wa ukusanyaji damu salama.

Kwa upande wa Halmashauri zote nchini Tanzania:

Kwanza, nichukue fursa hii kuzipongeza halmashauri zote ambazo zimetenga bajeti ya kukusanya damu kwa mwaka 2016/2017. Ni matarajio yangu kuwa, fedha hizo zitatumika kwa kazi hiyo muhimu iliyokusudiwa na siyo vinginevyo. Napenda kusisitiza kuwa ni jukumu la kila Mkoa/Halmashauri kuhakikisha hospitali zake zinakuwa na damu salama wakati wote. Pili, naagiza Mikoa/Halmashauri zote nchini kuweka utaratibu wa kufanya kampeni maalumu ya wiki moja katika kila robo mwaka ya kuhamasisha jamii juu ya uchangiaji wa damu, lengo likiwa ni kuleta hamasa ya wananchi kujenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara.

Tatu, nachukua fursa hii kukemea tabia ya baadhi ya watumishi katika hospitali zetu wenye tabia ya urasimu unaopelekea kuwepo kwa mianya ya rushwa katika kutoa huduma ya damu. Naagiza waganga wakuu wa Mikoa, Wilaya na Hospitali za binafsi kuhakikisha wanasimamia utoaji wa huduma ya damu bure kwa wananchi wote. Ninaagiza kuwekwa mabango katika Hospitali/vituo vya kutolea huduma za Afya vya Umma yanayoonesha kuwa damu ni bure na haiuzwi. Pia ninawaagiza viongozi wakuu wa Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo kinyume na maadili ya utumishi wa umma. Hata hivyo, ieleweke kuwa ndugu wa mgojwa wanaweza kutoa damu kwa hiari.

Mwisho, wakati tunaelekea kwenye kilele cha kuadhimisha siku ya wachangia damu duniani napenda kutoa rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili Taifa liwe na akiba ya damu ya kutosha na hatimaye kupunguza vifo ambavyo vinaweza sababishwa na ukosefu wa damu. Naomba niwahakikishie wananchi kuwa zoezi la kuchangia damu ni salama na halina madhara yeyote ya kiafya. Kwa akina mama wanaweza kuchangia damu mara tatu kwa mwaka na wanaume mara nne kwa mwaka. Nito rai kwa wananchi kuona kuwa kuchangia damu ni jambo jema, ni jambo la heri na ni jambo la kiutu kwa sababu tunaokoa uhai wa mtu.

Tufanye kazi kwa umoja na upendo katika jukumu hili la kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mwananchi mwingine anayehitaji damu na kuthibitisha kuwa: “SOTE TUNAUNGANISHWA NA DAMU (BLOOD CONNECTS US ALL)”

CHANGIA DAMU OKOA MAISHA

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA, 








All the contents on this site are copyrighted ©.