2016-06-11 06:49:00

Nguvu ya huruma na msamaha inashinda ubaya wa dhambi!


Mwandishi mmoja Anon anatushirikisha kuwa katika jarida moja la kila wiki la kanisa kulikuwa na mwaliko kwa waamini kushiriki ibada ya pamoja ya toba, na iliandikwa hivi: ‘kama huna dhambi yo yote, basi mlete rafiki yako mwenye dhambi’. Ndugu wapendwa, leo tunakutana tena pamoja kumshukuru Mungu kwa wema wake na kwa upendo wake kwetu sisi. Neno la Mungu leo latuelekeza kutafakari dhana ya dhambi na utakatifu, lakini zaidi sana twatafakarishwa juu ya ukuu wa huruma na mapenzi ya Mungu.

Tunasikia katika masomo yetu ya leo  jinsi ilivyo vigumu kwa mtu kutambua au kukiri dhambi au kuwajibika kwa makosa/dhambi zetu mbalimbali alizotenda. Mojawapo ya mifano iliyo wazi katika Biblia ni ile dhambi ya mfalme Daudi. Hata wakati nabii Nathan anamsimulia ule mfano, yeye hakung’amua kuwa ullimlenga yeye. Na jibu lake Daudi ni kuwa mtu huyo anastahili kufa. Ni baada tu ya nabii kumwambia kuwa mtu huyo ni wewe, basi anarudi katika fahamu zake. Bahati yake Daudi alikiri kosa lake na kuomba msamaha.

Ila jambo jema zaidi ni pale tu anapoomba msamaha kwa kosa hilo. Wengi wetu tunashindwa hapo hata baada ya kuelezwa makosa yetu bado tunakataa hilo. Baada ya ungamo hilo, Nathani anamtangazia msamaha. Hapa tunaona ukuu wa Mungu, mwingi wa huruma na msamaha – Zab. 136. Mungu hapendi kifo cha mwenye dhambi.

Ni kwa nini inakuwa vigumu mtu kutambua au kukiri au kubeba majukumu hasa pale anapotenda dhambi? Padre Munachi, mhubiri maarufu anarahisisha jibu akisema angalia ilivyo vigumu kwa mkoramaji kujua au kukubali kama ni mkoramaji. Wengine watakusikia isipokuwa mkoramaji hawezi kujisikia na hata akiambiwa huwa anabisha.

Mwanafalsafa Socrates anasema kuwa mtu ambaye hana tafakari ya maisha yake hafai kabisa kuishi. Tulipoadhimisha sherehe ya Ekaristi Takatifu, tulifafakarishwa nafasi ya kumbukumbu katika maisha. Bila kumbukumbu tungepoteza umimi wetu, kitambulisho binafsi. Mwenye ugonjwa wa amnesia – hupoteza kabisa mwelekeo, hajui alipo, hana kumbukumbu na hata hajui jina lake au alipo. Kumbukumbu ikiungana na akili inaelekea kitu Fulani halisi. Utajiri wa mtu, familia, kabila, taifa haupimwi na wingi wa dhahabu bali wingi wa kumbukumbu walizo nazo katika dhamiri na matendo yao. Hatari ya kumbukumbu ni pale inapokuwa ng’ang’anizi. Kulazimisha mambo au kufanya kwa mazoea. Huyu farisayo anafanya kile alichozoea.

Mfalme wa Urusi alitaka kutoa msamaha kwa wafungwa wake. Akatembelea gereza kuu la mji wake na akaongea na mfungwa mmoja baada ya mwingine. Wote isipokuwa mmoja alitamka wazi makosa yake. Mara moja mfalme akaamuru askari jela amfungue huru mfungwa yule. Wote walishangaa. Mfalme akasema huyu amekiri kosa lake na hana haja ya kukaa hapa. Amejitambua na anastahili kuwa huru. Wengi wetu tunakwama hapa.

Katika injili tunasikia habari ya farisayo, mwanamke mzinzi na Yesu. Yule Farisayo anamshangaa Yesu kwamba hajui kwamba yule mwnanamke ni mwenye dhambi. Anadhani kwamba Yesu anakaa kimya juu ya dhambi, kwamba anaunga mkono dhambi. Mtoto mmoja akiwa anasali sala ya Baba Yetu usiku kabla ya kulala alisikika akisali – na utuasemhe makosa yetu kama tumwasemehevyo waliokufa dhidi yetu.         

Shida ya yule Farisayo ni uelewa wake wa dhambi na utakatifu. Kadiri yake yule mwanamke ni sababu ya dhambi hivyo mtu wa Mungu au watu wa Mungu wakae mbali naye. Yesu anamsahihisha akisema kuwa la msingi si kuepuka bali kinachogomba ni kile utendacho. Kwa uhakika Wafarisayo waliepuka mazingira ya dhambi, lakini hawakufanya la pekee kuwasaidia waliowaona kuwa wadhambi. Waliwatenga. Hili ndilo kosa la yule Farisayo. Kwamba yule mwanamke alikuwa mdhambi au dhambi aliitendea mahali gani si juu yetu. Pia si kwamba Yesu hakusema kuwa yule mwanamke hakuwa mdhambi.

Dhambi ya yule Farisayo ni kuona dhambi ya mwingine lakini kutokuwa tayari kutambua uwepo wa ukuu wa Mungu. Ufahamu wake na uelewa wake haukuvuka hali yake na uelewa wake wa mafundisho yake. Ndiyo maana Yesu anasema wazi kuwa dhambi ya yule farisayo ilizidi ile ya yule mwanamke – Lk. 7:44. Yesu anasema wazi kuwa amekuja ili kutibu. Mungu anachukia dhambi lakini anatoa nafasi kwa mdhambi kutubu dhambi zake.

Ndugu zangu tukumbuke kuwa haitoshi tu kusema mimi sijatenda, sitendi dhambi hii au ile. Kilichopo mbele yetu ni je ni kwa kiasi gani tumefanya mapenzi ya Mungu? Tukumbuke kuwa yule mwanamke mdhambi alimhudumia Yeu. Na Yesu anatambua haya matendo ya nje ya yule mwanamke. Na kwa kuwa karibu na Yesu anapata upendeleo. Yule aliyedhani kuwa hana dhambi hapati huo upendeleo wa Mungu ingawa kila siku anashika amri kadiri ya mafundisho yake. Yesu anamwambia imani yako imekuokoa. Yule mwanamke alitambua nguvu na huruma ya Mungu inayoshinda dhambi zake. Ni lazima neno la Mungu liwekwe katika matendo.

Ndugu zangu, katika mwaka huu wa jubilei ya huruma ya Mungu na tukifafakarishwa na neno la Mungu dominika hii ya leo tunaalikwa kuwa watu wa matendo na tunawajibishwa kuishi neno la Mungu kwa matendo. Tukjikumbushe yale yatupasayo kufanya ili tuipate hiyo huruma ya Mungu. Yako matendo ya nje ya kimwili ya huruma – kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu na matendo ya huruma ya kiroho ambayo ni kuwashauri wenye mashaka, kuwaelekeza wasiojua (wajinga), kuwaonya wadhambi, kuwafariji walioonewa, kuwasamehe wakosefu, kuwavumilia wakorofi na wasumbufu na kuwaombea wazima na wafu. Tukifanya hivi tutavuka hali ya yule farisayo na kutenda tendo la huruma kama alivyofanya yule aliyeonekana mdhambi.

Mtakatifu Maria Goretti aliuawa akiwa na miaka 11 kwa sababu alimkatalia mbakaji wake hitaji lake ovu. Huyo alimchoma kisu na kumwua. Akiwa anakata roho Maria Goretti alisali hivi “Ee Mungu msamehe kosa lake. Namtaka mbinguni”. Nguvu ya msamaha inashinda ubaya wa dhambi. Huu ndio utakatifu wa kimungu.  

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.