2016-06-11 07:45:00

Mawasiliano yasaidie mchakato wa kudumisha: haki, amani na upatanisho!


Tume ya Mawasiliano ya Jamii ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, CEPACS imehitimisha mkutano wake huko Accra, Ghana uliofanyika kuanzia tarehe 6- 9 Juni 2016. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya kisasa ili kuendeleza Uinjilishaji Barani Afrika kwa kutoa kipaumbele katika: Haki, Amani, Upatanisho na Maendeleo”.

Mkutano huu umewashirikisha wadau mbali mbali wa vyombo vya mawasiliano ya jamii kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika wakiwa na lengo la kuchangia mchakato wa maboresho ya njia ya za mawasiliano ili kukidhi utume na maisha ya Kanisa Barani Afrika hususan katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Waraka wake wa Kitume, Dhamana ya Afrika kwa kulitaka Kanisa Barani Afrika kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho!

Katika tamko la CEPACS baada ya mkutano huu, wajumbe wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wa Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Duniani kwa mwaka 2016 uliosomwa na Askofu mkuu Jean- Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Ghana. Wajumbe wanaunga mkono mchakato wa maboresho unaoendelea kufanywa na viongozi wa CEPACS na kwamba, umefika wakati hata kwa Mabaraza ya Maaskofu Kitaifa na Kikanda kufanya maboresho makubwa katika Idara za Mawasiliano ili kuweza kukidhi changamoto za mawasiliano Barani Afrika. Ili kufanikisha lengo hili kuna haja pia kwa Idara hizi kujenga na kukuza ushirikiano wa karibu ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina Barani Afrika.

Wajumbe wamepongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Habari Afrika, “CANAA” mradi ulioanzishwa na SECAM kwa mchango wake katika kuhabarisha. SECAM kwa wakati huu inaendelea kukusanya na kuhifadhi nyaraka za Kanisa Barani Afrika, juhudi zinazopaswa kuungwa mkono na wadau mbali mbali katika tasnia ya habari Barani Afrika. Wanataaluma wa tasnia ya habari wanahamasisha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii, ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mkutano huu umesimamiwa na Askofu Emmanuel Badejo, kutoka Jimbo la Oyo, Nigeria ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Askofu mkuu Jean –Marie Speich amewaambia wajumbe wa mkutano huu kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafuatilia kwa umakini mkubwa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika na kwamba, anatarajia kuona matunda mengi ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu SECAM ilipoanzishwa, kwa kuwa na utambulisho wake, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano mkuu wa SECAM utakaofanyika nchini Angola utaweza kuibua mbinu mkakati utakaoisaida SECAM kuwa na utambulisho wake makini.

Umefika wakati kwa Kanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba, linatumia njia za mawasiliano ya kisasa kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina kwa kuzingatia zaidi changamoto ya kukuza na kudumisha: haki, amani, upatanisho na maendeleo. Mababa wa Sinodi ya awamu ya pili ya Maaskofu wa Afrika walitaja mambo haya kuwa ni changamoto pevu kwa familia ya Mungu Barani Afrika, ili kuweza kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.